Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtuhumiwa wa ubakaji Krismasi alivyopunguziwa adhabu

HUKUMU Mtuhumiwa wa ubakaji Krismasi alivyopunguziwa adhabu

Mon, 25 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kama wewe ni mwanamke unataka kwenda kusherehekea leo sikukuu ya Krismasi sehemu yoyote ya starehe basi soma kisa hiki kilichotokea Kigoma mwaka 2019.

Mnamo Desemba 25, 2019 Kama ilivyo kwa watu wengi duniani, mwanamke mmoja ambaye jina lake kwa simulizi hii tutamuita Sikujua (sio jina lake halisi) alisherehekea sikukuu ya Krismasi mwenyewe na alifanya hivyo kwa kuchagua njia zake mwenyewe ili kuifanya siku hiyo iwe maalumu kwake.

Sikujua aliamini kwamba kileo kilikuwa kinywaji pekee kinachoweza kuchangia furaha na raha yake, alikwenda kwenye klabu ya pombe za kienyeji karibu na Kijiji cha Kayonza katika Wilaya ya Kakonko, Mkoa wa Kigoma, ili kuzima kiu yake.

Baada ya kupata kileo kwa raha zake na kwa kuwa mumewe alichelewa kumchukua wakati usiku wa manane unakaribia, aliamua kwenda nyumbani kwa miguu. Akiwa kidogo amelewa na akiyumbayumba njiani kutoka upande mmoja kwenda mwingine, barabarani alikutana na wanaume sita ambao alisema walikuwa pamoja naye kwenye klabu aliyokuwepo yeye, mahakamani aliwatambua na kuwataja, akiwemo Majaliwa Chiza.

Katika usiku huo, wanaume wale sita walimsimamisha na kumpeleka kando ya barabara kwa nguvu ambapo kwa zamu walimbaka mwanamke huyo.

Wakati wakitekeleza tendo hilo mwanamke huyo alipiga kelele ili asikike na kupata msaada kwa mpita njia yeyote ili anusurike kubakwa.

Kwa bahati nzuri mpita njia aliyetambulika kwa jina la Justine Msafiri alikuwa karibu na eneo la tukio, alifuata kelele zilipokuwa zinatokea na alipofika alifanikiwa kumkamata mshtakiwa mmoja ambaye alikuwa katika harakati za kuvaa suruali ili atoroke kama walivyofanya wenzake watano.

Baada ya kumkamata mshtakiwa huyo, Justine Msafiri alipiga simu kwa rafiki yake wa karibu ambaye naye aliwapigia simu wengine na taarifa ikafika kwa Tobias Gabriel, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kijiji, kwa mujibu wa maelezo yake aliliarifu Jeshi la Polisi huko Kakonko.

Polisi walikwenda eneo la tukio mara moja na kumkamata mshtakiwa kwa kosa la ubakaji wa kundi.

Sikujua alipelekwa hospitali ambapo alifanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa kuwa amefanyiwa tendo la ubakaji.

Ofisa wa upelelezi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, aliyetambulika kwa jina la Koplo Hamisi, aliteuliwa kufanya uchunguzi wa kesi, alielezea jinsi alivyomkamata mshtakiwa Desemba 25, 2019 na kisha kumhoji.

Katika mahojiano kati ya Koplo Hamisi, mshtakiwa, alidai kwamba siku ile ya tukio anahisi alipoteza simu yake ya mkononi kwenye eneo la tukio. Hamisi aliamini simu ile itamsaidia katika upelelezi wake ilimlazimu kwenda eneo la tukio na aliikuta simu hiyo kisha akaichukua.

Kulingana na maelezo na ushahidi huo, mshtakiwa alipatikana na hatia ya ubakaji wa kundi kinyume na vifungu namba 130(1) na (2) (a) na 131A (1) na (2) vya Kanuni ya Adhabu (Sura namba 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019) katika Mahakama ya Wilaya ya Kibondo.

Baadaye, alihukumiwa kifungo cha maisha kulingana na sheria. Hakuridhika na maamuzi ya Mahakama ya Wilaya ya Kibondo mshtakiwa huyo alifanikiwa kukata rufaa Mahakama Kuu lakini pia rufaa ilikataliwa, mtuhumiwa huyo bado hakukata tamaa aligonga hodi milango ya mahakama ya rufaa (huu ndio ulikuwa ukingo wa Majaliwa Chiza).

Katika rufaa aliyoikata katika awamu hii, Majaliwa alimkosoa jaji aliyemuhukumu awali kwa sababu tatu.

Mosi, kuthibitisha hatia na hukumu bila kuwepo kwa ushahidi thabiti unaothibitisha kosa bila shaka yoyote;

Pili, kuthibitisha hatia na hukumu wakati akitegemea hati ya mashtaka batili isiyofaa na isiyoelezea vizuri vipengele vya kosa; na Tatu, kuthibitisha hatia na hukumu bila kuzingatia kwamba mshtakiwa hakutambuliwa kwa usahihi.

Itambulike kwamba ni haki ya kikatiba kwa kila Mtanzania kupata uwakilishi wa wakili na kama huna uwezo basi Serekali itakupatia mmoja lakini haki hii haikuzuii wewe kujiwakilisha mwenyewe.

Mshtakiwa alijitetea bila uwakilishi wowote akichuana na mawakili wa Jamuhuri. Mahakama ilimruhusu Majaliwa kufafanua misingi ya rufaa yake. Alitoa hoja za rufaa na mawakili wa Serikali wakazijibu.

Baada ya hapo alitoa majumuisho ya kimsingi akisisitiza kwamba kosa halikuthibitishwa kufikia kiwango kinachohitajika.

Hata hivyo, hoja za Majaliwa hazikuweza kusaidia rufaa yake na zilikuwa kiujumla nje ya mwelekeo. Kwa mfano, alilalamika kwa nini Sikujua hakutoa ushahidi kama shahidi wa kwanza katika kuthibitisha kesi ya upande wa mashtaka; na kwa nini Sikujua hakutoa nguo za ndani zilizoraruliwa kuonyesha kwamba kweli alibakwa, lakini katika kuthbitisha kesi ya ubakaji wa kundi hivi si vipengele vya uthibitisho katika kesi.

Mshtakiwa pia aliibua swali moja ambalo Mahakama ilijiridhisha na kujiuliza “Uaminifu wa Sikujua kama shahidi pekee wa tukio.”

"Je! Sikujua alikuwa na saa ambayo alikuwa akiangalia kila baada ya muda ili kubaini kwamba kila mmoja wetu alitumia takribani dakika tano kumbaka?" alihoji Majaliwa.

Katika kupinga rufaa hiyo, wakili wa Serikali alidai kwamba Majaliwa Chiza alitambuliwa ipasavyo kwani alikamatwa dhahiri katika eneo la tukio, hivyo swali la kutotambulika kwake halina miguu ya kusimama mahakamani. Kwa kusisitiza zaidi, wakili wa Serekali alisema mahakama ilishawahi kutoa uamuzi kama huo na ilisema kwamba “ushahidi wa kweli wa ubakaji lazima utoke kwa mwathiriwa (aliyebakwa)” pia mahakama ilitoa kanuni kwamba “kila shahidi anastahili kuaminika na lazima aaminiwe na ushahidi wake kukubaliwa, isipokuwa kama kuna sababu nzuri na thabiti za kutokuamini.”

Katika utambuzi wa mtuhumiwa kwenye tendo la ubakaji, mahakama ilikuja na mawazo tofauti kwani kesi hii ni tofauti na kesi nyingine zilizokwisha amuliwa katika ushahid wa mazingira, utambuzi katika kesi hii Majaliwa Chiza alipatikana na kukamatwa akiwa ameshusha suruali yake chini.

Mbali na hapo mahakama ilisema ikizingatiwa kwamba Sikujua alikuwa mlevi, ushahidi wa Koplo Hamisi ambaye alimkamata Majaliwa Chiza akiwa ameshusha suruali yake unapaswa kuwa pigo la mwisho kwa kesi hii.

Kuhusu nguzo ya pili ya rufaa ya Majaliwa Chiza, yakumkosoa jaji kwamba alitibitisha hatia na hukumu kwa kutegemea hati ya mashtaka isiyofaa, ambayo haikufichua vipengele vya kosa la ubakaji wa kundi, tujikumbushe kidogo nini sheria inasema kuhusu jinai ya ubakaji wa kundi.

kifungu cha 131 A (1) cha Kanuni ya Adhabu kinasema kwamba: "Mahali kosa la ubakaji linapofanywa na mtu mmoja au zaidi katika kundi la watu, kila mtu katika kundi linalofanya au kuchochea kufanyika kwa kosa hilo anachukuliwa kufanya ubakaji wa kundi."

Shauri hili lilipokuwa Mahakama Kuu, iliweza kuthibitisha kwamba Sikujua alibakwa na Majaliwa Chiza pamoja na wanaume wengine watano, ambao hawakushtakiwa kwa kuwa walifanikiwa kutoroka.

Hata hivyo, Justine Msafiri aliiambia Mahakama kwamba wakati anawasili eneo la tukio kulikuwa na wanaume wawili tu, mmoja wao akisimama na mwingine akiinama. Walipomwona akikaribia, yule aliyekuwa amesimama alikimbia wakati yule aliyekuwa akiinama, ambaye, kama ilivyobainika, alikuwa Majaliwa Chiza, alijaribu kuvaa suruali yake lakini Justine Msafiri alikimbia kwa haraka na kumkamata.

Muongozo wa Mahakama

Sheria inasema kuwa, uwepo tu wa mshtakiwa mahali pa tukio la kosa hautoi sababu ya kutosha ya kuthibitisha hatia ya mshtakiwa. Zaidi mahakama ilishawahi kusema kwamba "...hakuna kosa la jinai kusimama tu, kuwa shuhuda wa kosa, hata kama ni mauaji; kutofanya kitu kuzuia kosa si kosa lenyewe…”

Kwa kuwa mshikwa na ngozi ndiye mla nyama na kama ulivyotolewa ushahidi hapo awali Mahakama Kuu, palikuepo wanaume wawili na mmoja wapo alitoroka baada ya kumuona Msafiri anamkaribia pia hakukuwa na ushahidi wa kuthbitisha ushiriki wake halisi katika utekelezaji wa kosa lililo mbele ya mahakama. Mahakama ya rufaa ilifuta hatia ya ubakaji wa kundi na kubadilisha kuwa na hatia ubakaji, kinyume na kifungu cha 130(2)(a) cha Kanuni ya Adhabu.

Maamuzi ya Mahakama ya Rufaa

Kwa mamlaka ambayo Mahakama ya Rufaa inayo ilibatilisha kifungo cha maisha alichohukumiwa Majaliwa Chiza na badala yake kikawa kifungo cha miaka 30 jela kulingana na kifungu cha 131(1) cha Kanuni ya Adhabu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live