Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtuhumiwa mauaji kumchinja bibi mbaroni

RPC MBEYA SACP ULRICH MATEI (1)(1) Mtuhumiwa mauaji kumchinja bibi mbaroni

Tue, 28 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JESHI la Polisi mkoani Mbeya, limemkamata mtuhumiwa Hakimu Mwakifuna (20), mkazi wa Kijiji cha Nkunga, Kata ya Kiwira wilayani Rungwe kwa madai ya kumuua bibi yake, June Sankanye (55) kwa kumkata kichwa kisha kukibeba kwenye ndoo na kutokomea nacho kusikojulikana.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, Ulrich Matei, alisema Aprili 21, mtuhumiwa alifukuzwa nyumbani kwa bibi yake ambaye ni mzaa mama yake baada ya kuanza kuwatisha ndugu zake kuwa atawauwa kwa kutumia panga.

Siku mbili baadaye alienda kukaa kwa bibi yake mzaa baba ndipo alipofanya unyama huo wa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni na kutokomea na kichwa chake mahali kusikojulikana.

Vile vile, Kamanda Matei alikanusha uvumi kuwa mtuhumiwa huenda ana matatizo ya akili ndiyo sababu ya kufanya unyama huo na kudai kuwa suala hilo liko mikononi mwa vyombo vya sheria hivyo visiingiliwe na atapandishwa kizimbani muda wowote kujibu tuhuma hizo.

"Siamini kabisa kama huyo mtuhumiwa ni mgonjwa wa akili, maana baada ya kumbana alituonyesha wapi alikiweka na kichwa cha bibi yake na kukikuta kimeviringishwa kwenye mfuko wa sandarusi, sasa utawezaje kusema huyu mtu ana tatizo la akili," alisema Matei.

Familia ya marehemu Sankanye ilielezea tukio hilo ambayo ilimzika marehemu bila kichwa, ilidai kulazimika kuufukua mwili na kuuzika upya baada ya kichwa chake kupatikana kikiwa kimetelekezwa ndani ya ndoo, kwenye Pagara lililopo eneo la Ilundo.

Msemaji wa familia, Harun Mwakatumbula, alisema bibi huyo aliuawa na mjukuu wake, Aprili 23, majira ya saa 11 alfajiri kwa kuchinja kichwa kwa kutumia panga.

Alisema familia kwa kushirikiana na wakazi wa Kijiji cha Nkunga, walifukua kaburi ili waunganishe kichwa na kiwilili na kuzika pamoja.

Alisema kichwa kilipatikana baada ya mtuhumiwa wa mauji hayo ambaye anadhaniwa kuwa na tatizo la afya ya akili kukamatwa katika eneo la Kiwira na kwenda kuonyesha sehemu alipokitelekeza.

Dada wa mtuhumiwa, Julius Mwamloka, alisema mdogo wake alikamatwa eneo la Kiwira, wakati alipoenda kwenye nyumba ya mtu mmoja kuomba maji ya kunywa, na mtu huyo alitoa taarifa baada ya habari zake kuenea maeneo yote ya kata hiyo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mariam Nurdin, alikiri kufukuliwa kwa kaburi la marehemu na kuzikwa upya baada ya kichwa chake kupatikana.

Alisema mtuhumiwa alikitelekeza kichwa hicho kwenye pagala, sehemu ambayo watu wanachimba mchanga, aliwashukuru wananchi wa kijiji hicho kwa ushirikiano waliotoa na kueleza kuwa ni tukio la kwanza na la aina yake kutokea eneo hilo katika kijiji chake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live