Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtuhumiwa adaiwa kufia mahabusu polisi

Mtuhumiwa Afia Polisi Charles Owenya (50) mkazi wa Msaranga anadaiwa kufia mikononi mwa polisi

Tue, 6 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Matukio ya raia kudaiwa kufa wakiwa mikononi mwa polisi yanazidi kusikika nchini na safari hii, mkazi wa Msaranga katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Charles Owenya (50) anadaiwa kufariki dunia akiwa kituo cha polisi Majengo.

Hili ni tukio la nne katika kipindi cha miaka minne cha ndugu kudai ndugu zao waliokamatwa katika wilaya za Mwanga, Rombo na Moshi wakiwa hai, lakini baadaye kuambiwa wamefariki dunia.

Septemba 2018, Henry Kiwia aliyekuwa dereva wa daladala mjini Moshi, alidaiwa kujinyonga akiwa mahabusu kituo kikuu cha polisi Moshi na ndugu walipinga sababu zilizotolewa na polisi.

Ukiacha tukio hilo, Aprili 2019, kijana Waziri Mlacha alidaiwa kuuawa kwa kipigo cha polisi katika kituo cha Kisangara wilayani Mwanga, lakini polisi wakatoa taarifa iliyopingwa na ndugu kuwa alikufa kwa ugonjwa wa kifafa.

Pia Septemba 2022, mkazi wa kijiji cha Kirongo ya chini wilayani Rombo, Ulirki Sabas naye alidaiwa kupigwa na polisi wa kituo cha Usseri na kupoteza maisha akiwa mikononi mwao, lakini polisi wakadai amekufa kwa ugonjwa wa kifafa.

Septemba 2022, mkazi wa kata ya Njoro, mjini Moshi, Nicholaus Mushi (27) alidaiwa kujinyonga kwa kutumia tambara la deki akiwa mahabusu kituo kikuu cha polisi alikokuwa akishikiliwa kwa tuhuma za wizi wa simu na kompyuta.

Mbali na matukio hayo ya mkoani Kilimanjaro, pia kumekuwepo na matukio yanayofanana na hayo ya watuhumiwa kukamatwa wakiwa wazima, lakini baadaye kudaiwa kufa wakiwa mikononi mwa polisi, wengine wakidaiwa ni kwa kipigo maeneo mbalimbali nchini.

Tukio la Moshi lilivyokuwa

Taarifa zinadai Desemba 2, 2022, Owenya alikamatwa nyumbani kwake Msaranga na kupelekwa kituo cha polisi Majengo huku ikielezwa kuna baadhi ya vijana walimpa mzigo wa sabufa awahifadhie nyumbani kwake.

Kulingana na taarifa hizo, Polisi wakati wakiendesha msako wa kuwasaka washukiwa wa wizi huo, walifanya upekuzi kwa Owenya na inadaiwa alikutwa na vitu hivyo vikiwa ndani kwake na ndipo polisi walipomtia mbaroni.

Akisimulia tukio hilo jana, mtoto wa marehemu, Samweli Owenya alisema Ijumaa ya Desemba 2, askari waliokuwa wamevalia sare za polisi na kiraia walitoka nyumbani kwa baba yake na kuondoka naye muda wa alfajiri.

Alisema Desemba 3, askari walipiga simu nyumbani kwao na kueleza baba yao amefariki dunia, jambo ambalo alisema wao kama familia hawakulielewa Jeshi la Oolisi kwa kuwa ndugu yao alikuwa mzima na hakuwa na maradhi yoyote.

Inadaiwa polisi waliwaeleza ndugu hao amekufa kwa ugonjwa wa kisukari, sababu ambazo zinapingwa vikali na ndugu wa marehemu, huku wakimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume kuchunguza ukweli wa tukio hilo.

“Kama alikuwa anaumwa kwanini familia hatukupigiwa simu? Ni sawa amekufa, lakini amekufaje?

“Baba yetu hakuwahi kuumwa hata malaria na hakuwahi kuwa na ugonjwa wowote ni mtu aliuyekuwa na afya yake njema. Leo hii tunaambiwa amekufa, ni kitu ambacho hakituiingii akilini,” alisema mtoto wa marehemu na kuongeza:

“Baba yetu si kuku, polisi tunataka watuambie amekufaje wakati wao ndio walikuwa naye. Tunataka kujua kwanini amefia polisi na tunataka uchunguzi wa kina ufanyike tujue ukweli wa kilichotokea,” alisisitiza.

Kiini ni bodaboda

Mtoto huyo wa marehemu alidai kabla baba yake hajakamatwa, alifika kijana wa bodaboda akamuomba baba yake amhifadhie vitu hivyo na kwamba angekwenda kuvichukua siku inayofuata, ombi ambalo lilikubaliwa.

“Sasa kesho yake wakaja polisi nyumbani wakafanya upekuzi na kumkamata baba na vile vitu na wakamwambia kuna mahali kulivunjwa kukawa kumeibiwa wakamchukua wakaondoka naye,” alisema Owenya na kuongeza kusema:-

“Baada ya kumkamata wakamwambia awataje hao watu ambao walimletea hivyo vitu na yeye akawaambia hawajui kwa kuwa ni watu tu ambao amezoeana nao na walikuwa wanakaa wote kijiweni hajui wanapoishi, ni marafiki zake tu”.

“Sasa tunataka polisi watuambie wamemfanya nini huyu ndugu yetu maana wanachotuambiwa ni kwamba aliumwa kisukari, watuambie hicho kisukari kilitoka wapi na wakati baba hakuwahi kuumwa huo ugonjwa,” alidai Owenya.

Kwa upande wake akisimulia tukio hilo, mke wa mdogo wa marehemu, Melineema Owenya alisema shemeji yake alikamatwa alfajiri ya saa 11:15 na polisi hao wakaondoka naye.

“Asubuhi jana (juzi) tukawa tumempelekea chai tukaambiwa subirini na yule dada tuliyemtuma apeleke chai alisubiri sana pale kituoni bila kumwona akawaambia ana mtoto mchanga amemwacha nyumbani anataka kuondoka.

“Askari wakamwambia aende na aache chai watampa usafi ukishamalizika, basi yule dada akaacha akaondoka zake,” alisema.

Alieleza kuwa baada ya kuondoka familia walipigiwa simu kuwa ndugu yao amefariki dunia katika hospitali ya Mawenzi.

Alipotafutwa ‘In charge’ wa hospitali ya Mawenzi, Dk Edna Munis alimtaka mwandishi kufika katika ofisi za hospitali hiyo kupata taarifa zaidi. “Njoo kesho (leo) ofisini tutakupa mtu wa kulizungumzia hilo, sikuwepo ofisini.”

Chanzo: Mwananchi