Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto wa miaka 16, Kada wa Chadema wapotea mazingira yenye utata

36441 Pic+chadema Mtoto wa miaka 16, Kada wa Chadema wapotea mazingira yenye utata

Sun, 13 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mtoto Winn Mgeni (16), mkazi wa Tabata Aloma, jijini Dar es Salaam amepotea katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuondoka nyumbani kwao tangu Januari 4.

Mbali na Winn, mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) wilayani Ilala, jijini humo, Michael Kapama naye amepotea katika mazingira yenye utata Januari 6.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum Hamduni alipoulizwa kwa nyakati tofauti juu ya kupotea kwa Winne na Kapama alisema bado hajapata taarifa zao na kwamba anazifanyia kazi. Baba mzazi wa Winn, Nelson Mgeni akizungumzia kupotea kwa mwanae anayepaswa kuingia kidato cha tatu Midland ya jijini Dar es Salaam alisema siku ya tukio mwanae alitoka nje ya nyumba yao saa tano asubuhi na wote walijua hajaenda mbali.

Alisema walishangaa kuona saa zinapita hajarejea na walipojaribu kumtafuta kwa majirani kwa wakati huo hawakumuona.

Mgeni alisema ilibidi watoe taarifa kituo cha polisi cha Tabata- Shule ambako walifunguliwa taarifa namba TBT/RB/93/19.

“Siku hiyo alikuwa tu nyumbani mara akatoka nje, kwa sababu shule zilikuwa zimefunga tulijua yupo. Ila tukashangaa muda wa chakula cha mchana umefika haonekani, jioni haonekani ndio tukastuka,” alisema. Mgeni alisema licha ya kumtafuta kwa bidii huku wakiwaulizia ndugu, jamaa na marafiki ikiwa ameenda kwao hakukuwa na mafanikio yoyote

Baba huyo mzazi amewaomba watu watakayemuona popote alipo watoe taarifa kituo cha polisi kilicho jirani au kumpigia simu kwa namba 0757 74 5489.

Baadhi ya majirani walisema kwa tabia Winn ni mtoto mpole asiyependa kuongea hovyo na wakati mwingi hasa kipindi cha likizo hushinda nyumbani.

“Kwa kweli tumeshtushwa na kupotea kwa mtoto huyu, kama kuna mtu atamuona popote atupatie taarifa,” alisema Neema Mwenda, mkazi wa Aloma, Tabata.

Katika tukio la Kapama inadaiwa alitoweka tangu usiku wa Jumapili ya Januari 6 na kwa mara ya mwisho inaelezwa alionekana katika eneo la Kivukoni jijini Dar es Salaam, anakofanyia biashara.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema John Mrema alisema bado wanaendelea kumtafuta kada huyo na kwamba hakuna taarifa zozote zaidi walizonazo kuhusu kutoweka kwake.

Awali, Katibu wa Chadema jimbo la Ilala, Gervas Lyenda alisema alipata taarifa za kutoonekana kwa kiongozi jumanne jioni, baada ya ndugu kumtafuta bila mafanikio.

“Tuliambiwa toka Jumapili alipoondoka nyumbani kwake hakurudi tena na mpaka leo tunapoongea bado hajaonekana,” alisema.

Mwenyekiti wa Bavicha, Ole Sosopi aliomba jeshi la polisi kutoa taarifa ya haraka juu ya uchunguzi wao kuhusu kupotea kwa kada huyo.

“Aliyepotea ni raia wa Tanzania na kila Mtanzania ana haki ya kulindwa kwa mujibu wa katiba, sasa sio kwa sababu aliyepotea ni Chadema ndio wanyamaze,” alisema.

Waliowahi kupotea kwa nyakati tofauti na mpaka sasa hawajawahi kupatikana ni; Mwandishi wa Mwananchi wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani, Azory Gwanda na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Simon Kanguye.

Wengine ni Kada wa Chadema, Ben Saanane, Idrissa Ally (13) na Siri Nongwa wa miezi sita. Wote hawa ni wakazi wa Dar es Salaam.



Chanzo: mwananchi.co.tz