Mtoto wa miaka 15 anayeishi Kihesa Manispaa ya Iringa amedaiw akuwabaka na kuwalawiti jumla ya watoto 19 katika kipindi cha miaka minne.
Mtoto huyo amebainika jana Machi 14 baada ya Dawati la Jinsia la Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa usitawi wa jamii wa Manispaa na Mkoa huo kufanya oparesheni ya kuwasaka watuhumiwa wa matukio ya udhalilishaji.
Akielezea namna alivyogundua tatizo hilo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Igeleke, Sigfriend Mapunda alisema kuwa alimbaini mtoto mmoja darasani baada ya kuona anatoa harufu na kumhoji na kutaja watoto wengine waliokuwa wakifanyiwa vitendo hivyo.
"Nilimgundua mtoto mmoja baada ya mtoto mwenzie kuja kushtaki kwangu nikamuita nikamuhoji akakiri na kuwataja wenzake na wengine wengi hadi kufikia idadi ya watoto 19.
“Mtoto mwingine nilimuona ananuka anatoa harufu mbaya nikamuhoji na kukiri kufanyiwa kitendo cha udhalilishaji na kijana mwenye umri wa miaka 15 ambapo mtoto huyo aliwataja watoto wengine ambao wanafanyiwa vitendo hivyo," amesema.
Amesema baada ya kuwabaini watoto hao, waliwapigia simu wazazi wao badaye kwenda kuripoti tukio hilo polisi na kuwapeleka hospitali ambako walithibitika kufanyiwa vitendo hivyo.
"Tunawaomba wazazi wawe karibu na watoto wao wasiwaache watoto wakarubuniwa kwa kuangali TV na vizawadi vidogo vidogo wawe marafiki wa watoto wao ili linapotokea tatizo waweze kuwaelezea na kulichukulia hatua" amesema Mmoja wa wazazi mwenye mtoto aliyefanyiw aukatili amesema aligundua mtoto wake amefanyiwa vitendo hivyo wakati akimuogesha.
"Niligundua mtoto wangu wa kike kafanyiwa vitendo vya uzalilishaji wakati namuogesha akasema anasikia maumivu sehemu za siri ndio nikamuuliza akaniambia kilichotokea nikaamua kwenda kushitaki polisi na tukaenda kupima hospitali ikathibitika ni kweli ameingiliwa," amesema.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia la Polisi Mkoa wa Iringa, Elizabeth Swai amesema kutokana na ongezeko la ubakaji na ulawiti wa watoto mkoani humo, wameamua kufanya kampeni ya kupinga ukatili kwa watoto ili kunusuru watoto na kuondoka na janga hilo.
"Cha kusikitisha zaidi mtuhumiwa wa tukio hili ni mtoto, hivyo tumemuweka chini ya ulinzi wa Polisi ili kumlinda na hasira za wananchi wenye hasira kali baada ya kuona watoto wa wahanga wanasema kwa kuwa ni mtoto lazima tutamuachia hivyo atabaki na sisi polisi mpaka pale taratibu zingine zitakapofuata," amesema.
Amesema familia ya mtoto huyo inatambua tabia ya mtoto wao, kwa sababu alishawahi kumfanyia mtoto wa ndugu yake na kesi ilifika polisi na kumalizwa kifamilia na alifukuzwa shule aliyokuwa akisoma.
"Mtoto huyu awali alikuwa akiishi Semtema kabla ya familia yake kuhamia mtaa wa Kihesa Kilolo. Mwaka jana watoto 12 walifanyiwa unyanyasaji huo na baada ya kumuhoji alikiri kosa,” amesema.
Kwa upande wake ofisa Maendeleo ya Jamii wa mkoa huo, Sauda Mgeni alisema kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka kila mwaka ambapo kwa mwaka 2019 waliripotiwa watoto 404, waka 2020 watoto 439 na mwaka 2021 watoto 384 kwa mujibu wa watoto waliripotiwa polisi kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti.