Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto wa miaka 14 atuhumiwa kubaka, kulawiti ndugu wawili

Mbaroni Mtoto wa miaka 14 atuhumiwa kubaka, kulawiti ndugu wawili

Mon, 23 Oct 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mtoto wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) mkazi wa Kijiji cha Mnete, kilichopo Kitongoji cha Chiano, Kata ya Nalingu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwabaka watoto wawili wakiwemo binti wa miaka 7 na kumlawiti mtoto wa kiume wa miaka mitano.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Oktoba 23, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo imesema kuwa tukio hilo limetokea Oktoba Mosi na Oktoba 15, 2023 kwa nyakati tofauti mtuhumiwa anatuhumiwa kumbaka mtoto wa kike mkazi wa Nalingu na kumsababishia maumivu katika sehemu zake za siri.

Pia, mtuhumiwa huyo huyo kwa nyakati tofauti anatuhumiwa kumlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitano mkazi wa Nalingu na kumsababishia maumivu katika sehemu yake ya haja kubwa.

"Waathirika wote wawili wamefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na wanaendelea vizuri, mbinu iliyotumika ni kuwavizia nyakati za usiku wakiwa wamelala kisha kuwaingilia mmoja baada ya mwingine na kiini cha tukio ni tamaa za kimwili” amesema Kamanda Katembo.

Kamanda Katembo ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia pamoja na maadili yanayokinzana na sheria za nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari mapema, mama mzazi wa watoto hao, amesema siku ya Alhamisi Oktoba 19, 2023 akiwa kazini alipigiwa simu kuwa watoto wamevamiwa na mdogo wake wa kiume.

Amesema walipomhoji ameeleza huwa anawafanyia vitendo hivyo kila mara dada yake (mama mzazi wa watoto hao) anapotoka na kueleza kuwa kwa mtoto wa kiume alishamuingilia mara tatu ila wa kike ameshakuwa kama mke wake (anaumuingilia mara nyingi).

Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mnete, Halima Mohamed amesema baada ya kupata taarifa alizitoa kwa mgambo wa kata na kumueleza kuwa watoto hao wamekuwa wakibakwa na mjomba wao kila mara mama yao anapotoka kwenda kwenye shughuli zake za kujitafutia riziki, ambapo mjomba huyo huachiwa watoto hao kuwalea.

Amesema mtuhumiwa alipopelekwa ofisi ya kata na kuhojiwa alisema ni kweli amekuwa akiwafanyia watoto hao vitendo hivyo na huwapumzisha pale mama yao anaporudi nyumbani.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa walipomhoji mtuhumiwa, alikiri kuwa ni kweli amekuwa akiwafanyia vitendo hivyo vya kikatili watoto hao.

Chanzo: mwanachidigital