Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto wa miaka 12 afia bafuni, adaiwa kujinyonga

67693 Pic+mtoto

Mon, 22 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Kifo cha mwanafunzi wa darasa la sita Shule ya Msingi Uhuru iliyopo Manispaa ya Morogoro, Shabani Mashaka (12) kimeacha maswali na kuibua utata kutokana na mazingira yake.

Mwanafunzi huyo alikutwa amefariki Jumatano iliyopita majira ya saa 2 usiku kwenye bafu la nyumbani kwao maeneo ya Kihonda Manyuki alipokwenda kuoga wakati mama yake mzazi, Tasiana Kilian muda huo huo alikwenda dukani kununua vocha na mkaa.

Wakati kukiwa na utata huo, Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alisema jana kuwa kwa uchunguzi walioufanya wamebaini mwanafunzi huyo alijinyonga kwa kipande cha kanga akiwa bafuni.

Kamanda Mutafungwa alisema mbali pia walimuhoji mama wa mtoto huyo na mfanyakazi wa ndani na kuwaachia wakitaka kujua undani wa kujinyonga mtoto huyo.

Alisema katika mahojiano na mama wa huyo walibaini, mama huyo alimuonya mtoto wake kuacha tabia ya kucheza na watoto wa kike na baadaye akamtaka akaoge na yeye kwenda dukani na aliporudi mwanae alikuwa bado yuko bafuni ndipo alipousukuma mlango wa bafuni na kumkuta akiwa ananing’inia tayari ameshafariki dunia.

Alifafanua kuwa taarifa ya daktari imeeleza kuwa kifo cha mtoto huyo kilitokana na kukosa hewa baada ya kujinyonga.

Pia Soma

Kamanda Mutafungwa pia alisema kama kuna mtu mwenye taarifa zaidi aziwasilishe huku akisisitiza juu ya kuongezeka kwa matukio ya kukatisha uhai na kuitaka jamii kukaa na watoto na familia ili kutatua changamoto mbalimbali kabla mtu hajaamua kujitoa uhai.

Akizungumzia tukio hilo babu wa marehemu John Simba alisema alipata taarifa za kifo cha mjukuu wake akiwa jijini Dar es Salaam na hadi anazungumza na gazeti hili jana alikuwa hafahamu chanzo.

Baada ya uchunguzi wa kidaktari mwili wa Shabani ulisafirishwa kwenda kijiji cha Melela wilayani Mvomero kwa mazishi yaliyofanyika juzi.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, Diana Mwakyusa alisema kifo cha mwanafunzi huyo kimewapa simanzi na uchungu walimu na wanafunzi hasa aliokuwa akisoma nao darasa moja kutokana na utata na mazingira ya kifo hicho.

Alisema baada ya kupata taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo walimu walikaa na wanafunzi na kuzungumza nao ili waweze kupokea taarifa za kifo cha mwenzao lakini pia kujadili namna ya kushiriki mazishi.

Alisema marehemu alikuwa mtoto mwenye maendeleo mazuri darasani lakini pia alikuwa mwepesi kushiriki michezo na shughuli nyingine za kitaaluma.

Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Shebe Mlapakolo aliwataka wazazi na walezi kutenga muda kukaa na watoto wao. “Kifo ni fumbo na pia kinapangwa na Mungu lakini nipende kuwakumbusha tu wazazi na walezi tupende kutenga muda wa kukaa na kuzungumza na watoto wetu, tutabaini mengi mazuri na mabaya wanayofikiria ama kutenda,’’ alisema Mlapakolo.

Alisema yeye akiwa mwenyekiti wa kamati ya shule bado hajapata taarifa sahihi ya chanzo cha kifo hicho hivyo hana uhakika na yanayozungumzwa hadi atakapopata taarifa kutoka Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye dhamana kutoa taarifa hizo.

Baadhi ya wanafunzi waliokuwa wakisoma na Shabani walisema kuwa saa chache kabla ya kifo wakiwa shuleni walisoma, kucheza na kula naye na alikuwa mwenye furaha na amani kama ilivyo siku zote.

Hadija Rajabu, mmoja wa wanafunzi waliokuwa wakisoma na marehemu alisema ameshtushwa na kifo hicho na kwamba hawawezi kumsahau kwa haraka kwa kuwa Shabani alipenda kushirikana na wanafunzi wenzake na hakuwa mgomvi.

Kufuatia kifo cha mwanafunzi huyo mkuu wa wilaya ya Morogoro Regina Chonjo alisema amesikitika kwani ndoto za mwanafunzi huyo zimekatika ghafla.

Chonjo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya, alisema kutokana na kifo hicho cha utata polisi ndio wenye mamlaka kuchunguza na kutoa taarifa sahihi ili jamii iweze kuondokana na utata huo.

Chanzo: mwananchi.co.tz