Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto wa Waziri Simbachawene kuburuzwa mahakamani

Simbachawene Mwanaye Mtoto wa Waziri Simbachawene kuburuzwa mahakamani

Tue, 23 Aug 2022 Chanzo: Mwananchi

Siku moja baada ya kusambaa video inayomuonyesha mtoto wa Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene akitoa lugha chafu mbele ya askari wa usalama barabarani, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema sheria itafuata mkondo wake.

Juzi ilisambaa video hiyo ikionyesha watu wanaolalamikia magari yao kugongwa na kijana huyo aitwaye James Simbachawene aliyekuwa akijitapa hawezi kufanywa chochote kwa kuwa ni mtoto wa waziri.

Kulingana na watu hao, kijana huyo alidaiwa kuzidiwa na ulevi na ndio maana aligonga gari zaidi ya moja na kuendelea na safari yake bila kujali.

Kipande kingine kilimuonyesha James akiwa kituo cha polisi na akibishana na askari waliokuwa kituoni hapo na kuwatolea lugha chafu huku naye akilalamikia kutaka kupigwa.

Kamanda Muliro alilieleza Mwananchi kuwa hakuna uhusiano wa kosa alilofanya kijana huyo na kuwa mtoto wa waziri, hivyo atawajibishwa kulingana na sheria.

“Katiba yetu ipo wazi. Ipo ibara inayosisitiza usawa mbele ya sheria.” Watu wote wapo sawa mbele ya sheria. Atashughulikiwa kama yeye. Kwenye kosa alilolitenda, kalitenda yeye. Hakuna uhusiano wa makosa aliyoyatenda na kumhusisha baba yake. Atawajibika kisheria kama yeye,” alisema Muliro ambaye kwa sasa yupo likizo.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi kanda maalumu, William Mkonda alisema upelelezi unaendelea na muda wowote atafikishwa mahakamani.

“Ni tukio la uvunjaji wa sheria za usalama barabarani lilitokea maeneo ya Oysterbay na alifikishwa kituo cha polisi Oysterbay. Tunakusanya ushahidi wote tukikamilisha atafikishwa mahakamani kesho au Jumatano,” alisema Mkonda.

Juzi jioni muda mfupi baada ya kusambaa kwa video hiyo, Waziri Simbachawene alitoa taarifa kukemea tukio hilo kwa kuandika, “Nimeiona clip inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii , nakiri kuwa huyo ni kijana wangu ambaye ni mtu mzima anajitegemea na anafamilia yake.

“Nimemwagiza mkuu wa kituo kwa sababu amekosa adabu kwa Jeshi la Polisi na ametenda kosa la usalama barabarani ashughulikiwe bila huruma kwa mujibu wa sheria. Binafsi naomba radhi sana kwa walioathirika na mkasa huo, lakini pia kwa jeshi la polisi na Watanzania wote. Poleni kwa usumbufu wowote mlioupata.”

Tukio hilo linaloendana na lililotokea mwaka 2016 ambapo askari wa usalama barabarani, Deogratius Mbango alijikuta katika vute nikuvute na mke wa aliyekuwa waziri Agustino Mahiga baada ya kumuandikia faini dereva wake kwa kosa la kutosimama kwenye kivuko cha watembea kwa miguu.

Taarifa zilieleza mwanamke huyo alimshambulia kwa maneno Mbango akieleza yeye ni mke wa waziri na hakubaliani na adhabu hiyo iliyotolewa kwa dereva wake.

Baada ya taarifa hiyo kusambaa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli alimpongeza askari huyo na kuelekeza apandishwe cheo kwa uthubutu aliofanya kusimamia misingi ya kazi yake.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa Serikali, na wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi, kilichofanyika mjini Dodoma, hayati Rais Magufuli alisema, “Ebo! Yule trafiki anajua kazi, mpandishe cheo. Na huyo waziri na mke wake nimeshamwambia.”

Chanzo: Mwananchi