Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto miaka 12 abakwa akitoka saluni kunyoa

Mtoto miaka 12 abakwa akitoka saluni kunyoa

Mon, 13 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka (12) amelazwa Hospitali ya Nyerere akidaiwa kubakwa na kijana mwenye umri wa miaka 25 wakati akitoka saluni kunyoa nywele.

Mama wa mtoto huyo, Shida Mwise aliyekuwa akimuuguza mtoto wake amesema leo kuwa tukio hilo lilitokea Januari 12, saa 10 jioni wakati mtoto huyo akitoka saluni kunyoa ndipo mtuhumiwa ambaye alimkamata kisha kumwingiza kichakani na kumbaka akimtishia kumchoma kisu kama atapiga kelele.

"Baada ya kumaliza haja yake alimtekeleza hapo kwa sharti la kutopiga kelele ambako mtoto huyo alijikokota hadi karibu na nyumbani akanguka.

Kwa mujibu wa mama huyo ndugu zake waliokuwa wanachuma mboga wakamwona na kumchukua huku nguo zote zikiwa zimelowa damu.

“Alipofika nyumbani akaanguka na kupoteza fahamu, baada ya kujulishwa taarifa hizo niliishiwa nguvu nikatoa taarifa kwa uongozi wa kijiji," amesema.

Amesema aliamua kwenda kituo kidogo cha Polisi Kenyana ingawa njiani alikutana na mtuhumiwa akataka kukimbia, lakini yeye hakumfuatilia kwa kuwa alikuwa anawahi polisi ili kupata msaada.

"Nilipewa PF 3 nikatafuta usafiri na kumleta hapa hospitali, mtoto wangu ameumizwa sana, mtuhumiwa mpaka asubuhi nauliza naambiwa hajakamatwa na yuko kijijini," amelalamika mama huyo.

Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Philipo Rhobi amekiri kutokea tukio hilo na kwa sasa wanamsaka mtuhumiwa.

"Jana sikupata taarifa mapema ningemnasa maana jioni alikuwa miongoni kwa watu waliopokea pembejeo za pamba, asubuhi nimewahi stendi kuona kama atatoroka hakuonekana, hivi naingia kwenye msako na mgambo wangu," amesema.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Tonte Wambura amesema wanamsaka mtuhumiwa ili akamatwe.

“Matukio haya yanazidi kushika kasi maana mmoja kafungwa miaka 30 hivi karibuni kwa kubaka mtoto mdogo," amesema.

Mmoja wa wauguzi ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema kuwa walimpokea mtoto huyo akiwa katika hali mbaya.

“Kwa ujumla amechanika sana ilibidi daktari achukue hatua za haraka kuingiza chumba cha upasuaji na kumshona sehemu zake za siri," amesema.

Polisi wilayani hapa wamesema wanafuatilia ili kumkamata mtuhumiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu amesema ameishawaagiza polisi na viongozi wa eneo hilo kushirikiana na wananchi ili kumkamata mtuhumiwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz