Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto apotea akiwa kanisani

Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mtoto wa miaka mitatu, Beauty Yohana amechukuliwa na mtu asiyejulikana bila ridhaa ya wazazi wake wakati mtoto huyo akiwa katika Kanisa la FPCT lililopo Mbezi Mwisho, jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea jana Septemba 23, 2018 wakati mtoto huyo alipokwenda kanisani na mama yake, Lucy Maganga na walipokuwa kanisani hapo, Beauty aliungana na watoto wenzake kwenye ibada ya watoto (Sunday school) wakati mama yake akiendelea na ibada.

Akisimulia mkasa huo, baba wa mtoto huyo, Yohana Isango amesema wakati watoto wakiendelea kujifunza, alitokea binti mmoja mweusi na kudai anamhitaji Beauty ili akampatie dawa.

“Mwalimu anasema kuna msichana alikwenda na kudai yeye ni mfanyakazi wa ndani na alimwambia Beauty anatakiwa akapewe dawa. Basi msichana huyo alimchukua mtoto na kuondoka naye,” anasema.

Anasema msichana huyo alimchukua na kuingia naye kanisani lakini baadaye alitoweka na mtoto huyo. Anasema baada ya ibada kwisha, mtoto hakuonekana na ndipo walipotambua kwamba ameibiwa.

 “Tulitoa taarifa kwenye kituo cha polisi cha Gogoni, Mbezi na leo asubuhi nimekwenda. Wameniambia wanaendelea na uchunguzi wa tukio hili,” amesema Isango ambaye ana watoto wawili, Bless na Beauty.

Alipoulizwa kuhusu kupotea kwa mtoto huyo, kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo amesema anazo taarifa hizo na kuwa jeshi la polisi linaendelea kumtafuta.

Atakayemuona mtoto huyo awasiliane na wazazi wake kwa namba 0652316007 au kutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi.

Chanzo: mwananchi.co.tz