Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto aliyetekwa kimafia arudi nyumbani baada ya siku 198

52164 Pic+idrissa

Mon, 15 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ni furaha iliyoambatana na machozi kwa wazazi wa Idrissa Ally (13), aliyetekwa kwa staili ya ‘kimafia’ na kurejea kwao juzi usiku ikiwa zimetimia siku 198 tangu alivyotoweka.

Idrissa ambaye ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia Ally kati ya watoto wawili alirejea juzi nyumbani kwao Tegeta Masaiti huku wazazi wake wakiwa hawana lile wa hili.

Mama mzazi wa Idrissa, Leila Kombe alisema hana mengi ya kuzungumza badala yake anamshukuru Mungu kwa mtoto wake kurudi salama kwa kuwa walikuwa katika kipindi kigumu.

“Kila kitu nilimuachia Mungu kwa kweli na amesikia kilio chetu hadi leo (jana)amepatikana.Baada kuingia ndani, Idrissa alikumbuka mdogo wake, ishak, na baiskeli aliyekuwa akiendesha kabla ya kutekwa.

“Pia aliniambia mama vipi shule nitarudi lini, maana nina hamu ya kuandika notisi kwa sababu sikuhudhuria vipindi,” alisema Leila huku akionekana mtu mwenye tabasamu.

Ally Idd, baba mzazi wa Idrissa aliungana na Leila kwa kumshukuru Mungu kwa mtoto wao kurudi salama.

Related Content

Asimulia Idrissa alivyorudi nyumbani

Ally alisema juzi jioni mama mzazi wa mtoto huyo, Leila Kombe alipokea ujumbe kutoka katika namba asiyoifahamu na kuelezwa kuhusu kutafutwa na mtoto wake.

Hata hivyo, hakuamini kwa kuwa ameshapokea ujumbe wa aina hiyo mara nyingi, kumtaka mume wake apige namba hiyo.

“Nilimpigia akaniambia yupo Ubungo na kwamba mtoto wake aliomba ampigie lakini ameshaondoka akielekea nyumbani kwao Tegeta,” alisema Idd.

Alisema hakuamini lakini ilikuwa kama miujiza saa moja usiku alisikia mlio wa pikipiki iliyoegeshwa nje ya nyumba yake ikiwa imempakia kijana wake.

“Bado siamini kama amerudi nyumbani, tumekuwa kwenye giza nene kwa muda mrefu.” Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kweli. Amepungua lakini amerefuka na ana nywele nyingi, inaonekana hakuwahi kunyoa tangu alipotekwa,” alisema Idd.

Kuhusu uwepo wake Morogoro, alisema hivyo ndivyo Idrissa alivyomueleza kwamba katika nyumba aliyokuwa akiishi ukutani kulikuwa na maandishi yaliyosomeka ‘Kilakala Morogoro’.

Alisema Idrissa amemueleza kuwa kuna kijana mmoja alimsaidia kumtorosha, alimpatia nauli akimtaka aende Dar es Salaam kwa wazazi wake.

Mwalimu wake azungumza

Mwalimu Mkuu wa Princes Gate, Mussa Idrissa alisema wamepokea kwa furaha taarifa za Idrissa kurejea kwani ni muda mrefu tangu alivyochukuliwa na watu hao ambao bado hawajafahamika.

“Amekosa muhula mmoja wa masomo, lakini tutawasiliana na ofisa elimu wa wilaya ili tujue namna ya kumsaidia kijana huyu kwa kuwa kesi yake inajulikana.

Alisema hivi sasa Idrissa inabidi atulie kupewa ushauri aweze kurudi katika hali ya kawaida na atakwenda kuzungumza wanafunzi wenzake kwa lengo la kuwajenga kisaikolojia kuhusiana na kurejea kwa rafiki yao.

“Tunataka Idrissa akiwa shuleni na darasani aonekane mtu wa kawaida tu badala ya wanafunzi wenzake kuanza kumhoji mara kwa mara likiwemo la ulikuwa wapi siku zote,” alisema Idrissa.

Mmoja wa majirani, Juvenile Bifa alisema wanafuraha kusikia mtoto huyo kurejea akiwa mzima na walitumia muda mwingi kumuombea Idrissa.

Jirani mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mama Shedrack, alisema alikuwa wa kwanza kupata taarifa za Idrissa kutekwa mwaka jana, lakini juzi usiku alikuwa mtu wa kwanza kumuona mtoto huyo akirejea nyumbani kwao.

“Niliona mtoto akishuka katika bodaboda sikujua kama ni yeye maana ni usiku, lakini uvumilivu ulinishinda nikasogea karibu na geti la kuingia ndani kwao na kujua kama ni yeye hakika Mungu ni mkubwa,” alisema.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu, Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuzungumzia kurejea kwa Idrissa, alisema hawezi kuelezea lolote hadi apate taarifa za kuridhisha kuhusu hatua hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz