Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto aliyeibiwa Bukoba apatikana Dodoma

Mtoto Aliyeibiwa Bukoba Apatikana Dodoma Mtoto aliyeibiwa Bukoba apatikana Dodoma

Mon, 12 Dec 2022 Chanzo: Eatv

Jeshi la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja Benita Beneti, ambaye aliibwa Desemba 01 mwaka huu katika mtaa wa Migera, Kata ya Nshambya katika Manispaa ya Bukoba, na kupatikana Desemba 08 mkoani Dodoma.

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera William Mwampaghale, amesema kuwa baada ya kuripotiwa kwa tukio hilo uchunguzi ulianza na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao katika maeneo tofauti, kuanzia Desemba 02 hadi Desemba 08 mwaka huu.

Kamanda huyo amesema kuwa baada ya mtoto huyo kuibwa na watuhumiwa hao walimpeleka kwa mganga wa jadi  katika eneo la Kamachumu wilayani Muleba, ili afanyiwe dawa asimsumbue anayemchukua.

Mara baada ya kutoka kwa mganga huyo wa jadi watuhumiwa hao walitawanyika, na mtuhumiwa aliyemchukua mtoto huyo aliondoka kuelekea Dar es Salaam, na wengine walijificha maeneo mbalimbali wakihofia kukamatwa.

"Msako uliendelea ambapo mtuhumiwa aliyekuwa amekimbilia Dar es Salaam, baada ya kugundua kuwa anafuatiliwa na polisi alikimbilia Dodoma kwenda kujificha, lakini ilipofika Desemba 08 mwaka huu saa 12:00 jioni tulimkamata," amesema Mwampaghale.

Naye mama wa mtoto huyo Johanitha Augustino amesema kuwa alipigiwa simu na polisi kuwa mtoto wake amepatikana na kumtaka ajiandae kwa ajili ya kumfuata mkoani Dodoma. 

"Tulianza safari ya kwenda Dodoma tulipofika pale tulikuta mtoto amekwishawekwa kwenye vipimo na mimi nikapelekwa kwenye vipimo, walipomaliza wakanikabidhi mtoto muda wa saa mbili asubuhi nikiwa na askari, wakanionyesha mtuhumiwa ndipo tukaanza safari ya kurudi Bukoba," amesema mama huyo.

Desemba 01 mwaka huu, watu waliowahi kuishi na mama wa mtoto huyo walifika mtaa wa Migera, Kata ya Nshambya kwa lengo la kumsalimia na mara ya watu hao kuondoka na kumtaka mama huyo awasindikize, aliporejea ndani hakumkuta mtoto wake na baada ya kumtafuta bila mafanikio aliripoti polisi na jitihada za kumtafuta kuanza.

Chanzo: Eatv