Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto ahoji kukaa mahabusu miaka miwili akisubiri kesi

Dhamana, Hukumu Mtoto ahoji kukaa mahabusu miaka miwili akisubiri kesi

Fri, 21 Apr 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mmoja wa watoto wanaohifadhiwa katika mahabusu ya watoto Upanga, jijini Dar es Salaam, amehoji kukaa mahabusu kwa miaka miwili sasa, akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake inayomkabili.

Mtoto huyo aliyekuwa mahabusu hapo kwa kukinzana na sheria akikabiliwa mashtaka ya mauaji, alibainisha hayo jana wakati wajumbe wa Tume ya Haki Jinai, iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuangalia namna ya kuboresha mfumo na taasisi zinazohusika na haki jinai ilipowatembelea.

Akizungumza na wajumbe hao, wakiongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu, Said Mwema, mtoto huyo alisema anakabiliwa na kesi ya jinai inayosikilizwa na Mahakama Kuu. Alisema amekaa mahabusu hapo kwa miaka miwili sasa akisubiri kesi yake hiyo.

“Mimi naitwa XY, nina kesi ya PI na mpaka sasa nina miaka miwili niko hapa kituoni. Lakini wanasheria wanaotutembelea wanasema kesi za watoto zinatakiwa kuisha ndani ya miezi sita. Tunaomba na sisi mtuangalie wenye kesi za aina hii,” alisema mtoto huyo.

Awali, meneja wa mahabusu hiyo, Darius Damas aliwaeleza wajumbe hao kuwa mahabusu ya watoto ilianzishwa mwaka 1962 kwa lengo la kuhifadhi watoto walioshtakiwa kwa kukinzana na sheria ili kuwapa mafunzo ya marekebisho ya tabia, wakati wakiendelea kusikiliza kesi zao mahakamani.

Alisema watoto wanaohifadhiwa kituoni hapo ni wale wanaokabiliwa na makosa ya mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi, kuingia nchini bila kibali. Damas alisema kesi za watoto zinapaswa kuisha ndani ya miezi sita na kama kuna sababu za msingi, inaenda hadi miezi tisa.

Akijibu maswali ya wajumbe, alisema hawana tatizo la kuchelewa kwa upelelezi, kwa sababu watoto hupelekwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika, isipokuwa kesi za mauaji, kwa kuwa hizo zina utaratibu wake maalumu.

Wakati huo huo, tume hiyo ilitembelea Chuo cha Taaluma ya Urekebu (urekebishaji tabia) cha Jeshi la Magereza Ukonga na kushauri kuweka mfumo wa kufuatilia mwenendo wa maisha ya watu waliomaliza vifungo vyao ili kujua kama wamekuwa wema kwa jamii. Ushauri huo ulitolewa na Mkuu wa Majeshi mstaafu, Inspekta Jenerali Ernest Mangu ambaye ni miongoni mwa wajumbe hao.

Awali, chuo hicho kiliwasilisha maoni yake yaliyojikita kwenye maboresho mbalimbali ya utendaji wa Jeshi la Polisi, ofisi ya DPP, mahakama, mfumo wa sheria, muundo wa taasisi ya magereza, uhaba wa bajeti na mahitaji ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Chanzo: mwanachidigital