Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto afariki kwa kukatwa mguu na mwenzake

Fri, 12 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Mtoto ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kisangura wilayani, Serengeti, Mchungure Mwita (14) amekufa baada ya kukatwa panga na mwenzake wakati wanachunga mifugo.

Mganga Mkuu wa hospitali Teule ya Nyerere, Emiliana Donald amesema chanzo cha kifo hicho ni mtoto huyo kuvuja damu nyingi.

Amesema mtoto huyo alipokelewa jana Oktoba 9, 2018, saa 8 au 9 akiwa anavuja damu nyingi na wakati wanamhudumia akakata roho.

"Baada ya kukatwa kwa panga huduma ya kwanza walifunga chini ya jeraha wakiamini wanazuia damu isitembee badala ya kufunga kwenye jeraha," amesema.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Enock Marwa amesema mtuhumiwa naye ni mtoto mwenye miaka 13 ambaye ametoroka baada ya tukio.

"Walikuwa wakichunga mifugo ikatokea kutokuelewana akamkata na panga tena kali na kusababisha damu kuvuja sana," amesema.

Amesema familia zao zinaishi jirani na hakuwahi kusikia kama wana mgogoro.

"Kila mmoja anajiuliza sababu za mauaji haya, aliyeuawa alikuwa anasubiri matokeo ya darasa la saba na mtuhumiwa yuko darasa la sita," amesema.

Polisi wilayani hapa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Chanzo: mwananchi.co.tz