Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtendaji kata, mwenyekiti watwangana ngumi

Mon, 23 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora. Kikao cha kujadili maendeleo ya kata, kimezua tafrani baada ya viongozi wawili; ofisa mtendaji kata ya Igunga mkoani Tabora, Robert Mwagala na mwenyekiti wa kitongoji cha Mwayunge, Abel Shampinga kupigana ngumi baadaye kuamliwa na wajumbe wa kikao hicho.

Viongozi hao waliamliwa na wenzao waliohudhuria kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo, hawakusababisha madhara kwao na wengine.

Akizungumzia ugomvi huo leo Julai 23, 2018, Mwagala amedai chanzo cha kupigana ni mwenyekiti huyo anayetokana na Chadema kuondoka na jalada lenye nyaraka za Serikali za mapato na matumizi ya kata.

Amedai baada ya yeye kusoma taarifa ya mapato na matumizi ya kata kwa wenyeviti wa vitongoji 16 na baadhi ya madiwani wa viti maalumu, Shampinga aliinua mkono kuomba kwa mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni diwani wa Igunga, kumruhusu kuchangia taarifa hiyo.

Ameeleza baada ya kuruhusiwa alidai taarifa hiyo haina ukweli kwani haiwezekani makusanyo ya ushuru wa vibali vya kupeleka ng’ombe mnadani ambao hutozwa Sh1,000 kila ng’ombe  na mbuzi Sh500 yawe Sh10,000 kwa wiki moja.

Ameendelea kuwa baada ya kumaliza kuchangia hoja, mwenyekiti huyo aliondoka na jalada hilo lakini alipomzuia mlangoni na kumtaka asitoke na jalada nje akugoma.

Ameeleza kuwa kugoma kwa mwenyekiti huyo ndiyo kulisababisha waanze kurushiana makonde na kuamliwa na wenyeviti wa vitongoji waliokuwapo.

Naye Shampinga amesema aliamua kubeba faili hilo kwa sababu kuna ufisadi uliofanywa na mtendaji kwenye makusanyo ya ushuru wa vibali vya mnadani.

Amesema licha ya kumzuia asibebe jalada hilo, suala hilo atalifikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa uchunguzi zaidi.

Diwani wa Igunga, Charles Bomani (CCM) amethibitisha viongozi hao kupigana ngumi kwenye kikao na kwamba, hakuna aliyejeruhiwa kwani wenyeviti wenzao waliwawahi kuwaamua na  kikao kiliendelea baada ya vurugu kutulia.

Bomani amesema kutokana na tuhuma dhidi ya mtendaji huyo kuhusu ushuru wa vibali vya ng’ombe, wenyeviti hao kwa pamoja waliamua kuunda kamati ya wenyeviti watatu ambao Jumamosi Julai 28, 2018 watafuatilia kujua mapato hayo mnadani ili kuona kama kuna ubadhirifu. 

Chanzo: mwananchi.co.tz