Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtawa aliyejiua Bugando ahusishwa uchunguzi PCCB Takukuru

16994 Pic+mtawaTanzaniaWeb

Fri, 14 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Kifo cha aliyekuwa mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Hospitali ya Rufaa Bugando ya jijini Mwanza, Sista Suzan Bartholomew bado kinajadiliwa na wengi, hasa kutokana na utumishi wake wa kiimani.

Sista Suzan alijiua kwa kujirusha kutoka ghorofa ya tatu ya jengo la hospitali hiyo Agosti 28.

Uamuzi wa Mtawa huyo kujitoa uhai saa 12:00 asubuhi, muda mfupi baada ya kutoka kusali uliwashtua watu wengi, hasa wale wa karibu waliofichua kuwapo kwa mwenendo wenye shaka na ishara kuwa angechukua uamuzi kama huo baada ya kudaiwa kugawa fedha na mali zake kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Kutokana na utata uliogubika tukio na kifo hicho, Mwananchi imegundua kuwa huenda mtawa huyo alichukua uamuzi huo kukwepa kuangukia kwenye mikono ya sheria kujibu tuhuma za ubadhirifu na upotevu wa mamilioni ya fedha.

Mtawa huyo pamoja na wenzake tisa kutoka idara ya fedha na vitengo vingine vya hospitali hiyo, wanachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za upotevu wa zaidi ya Sh316.3 milioni.

Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake, mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale alisema tayari taasisi hiyo imefungua jalada baada ya kufanya uchunguzi wa upotevu wa mamilioni ya fedha zinazotokana na malipo ya huduma kwa wagonjwa na wananchi wanaofika Bugando.

“Kweli tuna jalada la uchunguzi kuhusu upotevu wa fedha za Hospitali ya Bugando, ni bahati mbaya kwamba sista hayupo (amefariki dunia), lakini uchunguzi unaendelea na tumefikia hatua nzuri,” alisema Makale.

Ingawa hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa undani kutokana na kubanwa na sheria, uchunguzi wa Mwananchi umebaini Sista Suzan pamoja na wenzake wanadaiwa kuhusika na upotevu wa mamilioni hayo ya fedha.

Wakati mtawa huyo na msaidizi wake mkuu (chief cashier), wakibeba dhamana ya kiasi chote cha fedha zilizopotea kutokana na nafasi zao kiuongozi, watuhumiwa wengine (majina tunayahifadhi) wanadaiwa kuhusika na upotevu wa kati ya Sh2.2 milioni hadi Sh94 milioni, kila mmoja kwa kiwango chake.

Kwa pamoja, watuhumiwa hao wanadaiwa kuingiza na kuonyesha fedha hizo kwenye mfumo wa malipo ya Hospitali ya Bugando bila kuonekana kwenye akaunti ya taasisi hiyo.

Mkurugenzi afafanua

Akizungumza kwa simu, mkurugenzi mtendaji wa hospitalihiyo, Dk Abel Makubi alithibitisha kuwapo madai ya upotevu wa fedha katika taasisi hiyo inayomilikiwa na Kanisa Katoliki.

“Ni kweli uchunguzi unafanyika, siwezi kuzungumzia suala hilo kwa undani kwa sababu linachunguzwa. Labda polisi au vyombo vingine vya dola vinaweza kulizungumzia,” alisema Dk Makubi.

Mmoja wa wafanyakazi na mtu wa karibu na Sista Suzan aliliambia Mwananchi kuwa siku chache kabla ya kujiua, uongozi wa Hospitali ya Bugando ulimuondoa kwenye nafasi yake kupisha uchunguzi dhidi yake.

Habari za ndani zinasema kuwa wataalamu wanaendelea na uchunguzi wa kina kubaini ujanja uliotumika kufanikisha fedha kuingizwa na kuonekana kwenye mfumo wa malipo bila kuingia kwenye akaunti ya hospitali inayohudumia wagonjwa wa rufaa kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na zile za Magharibi za Tabora na Kigoma.

Kanda ya Ziwa inaundwa na mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Geita, Simiyu na Shinyanga.

“Inawezekana wizi huu una mtandao mkubwa hadi kwenye baadhi ya taasisi za fedha, nadhani mengi yatabainika na wengi kukumbwa,” alisema mmoja wa watoa taarifa kwa sharti la kuhifadhiwa jina.

Ingawa mkuu wa Takukuru Mwanza, Makale hakutaka kuingilia undani wa hatua iliyofikiwa katika uchunguzi unaoendelea, Mwananchi limebaini watuhumiwa wengine tisa wameendelea kuhojiwa hata baada ya kifo cha Sista Suzan.

“Mara ya mwisho watuhumiwa walihojiwa wiki iliyopita na inadaiwa waligoma kutoa maelezo ya ziada kwa kuweka msimamo wa kufanya hivyo mahakamani,” alisema mtoa taarifa wetu.

Imeelezwa kuwa kabla ya kujiuwa, Sista Suzan aliyezikwa Agosti 30 katika makaburi ya Kanisa Katoliki Kashozi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera alitoa ushirikiano kwa kueleza ukweli kuhusu upotevu wa fedha hizo.

“Kutokana na mwenendo wa uchunguzi, nyaraka na ushahidi, alihisi mzigo wa upotevu wa fedha hizo ulikuwa unamwelemea,” alisema mtu wake wa karibu.

“Nadhani ndiyo maana akachukua uamuzi wa kujiua kwa kujirusha kukwepa mkono wa sheria, alihisi ni fedheha yeye kushtakiwa mahakamani kwa wizi wa fedha za taasisi.”

Chanzo: mwananchi.co.tz