Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtandao wamrejesha mahabusu aliyemkata panga mwalimu

Mwanafunzi Auawa Kwa Kukatwa Mapanga.jpeg Mtandao wamrejesha mahabusu aliyemkata panga mwalimu

Wed, 4 Oct 2023 Chanzo: mwanachidigital

Alex Butawantemi, mwanafunzi wa shule ya sekondari Tamabu Wilaya ya Misungwi anayedaiwa kumkata kwa panga mwalimu, jana amelazimika kurejeshwa mahabusu ya polisi baada ya mtandao wa Mahakama kugoma kusajili kesi yake.

Mwanafunzi huyo anayeshikiliwa na polisi tangu Septemba 25, mwaka huu, anadaiwa kumshambulia kwa kumkata panga sehemu tofauti za mwili mwalimu Stanford Mgaya.

Baada ya kusota mahabusu kwa siku tisa tangu akamatwe, mwanafunzi huyo alifikishwa katika viunga vya Mahakama ya Wilaya ya Sengerema jana asubuhi tayari kusomewa mashtaka, lakini ilishindikana baada ya mfumo wa kusajili mashauri mahakamani hapo kugoma.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana Oktoba 3, 2023, Wakili wa Serikali, Morice Mtoi alisema baada ya mfumo wa usajili kugoma kutokana na tatizo la mtandao, aliwasiliana na uongozi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Sengerema ili mwanafunzi huyo arejeshwe mahabusu ya polisi.

‘’Hati ya mashtaka tayari imeandaliwa; tatizo lililokwamisha kesi ni usajili wa mtandaoni kugoma. Tunaendelea kufanya jitihada za kusajili na tunaamini kufikia jioni mtandao utakubali kwa sababu watu wengi watakuwa wametoka ofisini na mtandao kupata nguvu,’’ alisema Mtoi

Akifafanua, Wakili Mtoi alisema; ‘’Kwa kawaida, nakala ya hati ya mashtaka inayowasilishwa mahakamani lazima isajiliwe kwa njia ya mtandao katika mfumo wa usajili wa Mahakama ndipo Hakimu Mfawidhi atoe kibali kwa makarani kupokea, kufungua jalada na kutoa namba ya kesi,’’

Japo hajasomewa mashtaka, Wakili Mtoi alisema mwanafunzi Alex amefunguliwa kesi ya kujeruhi ambayo ndiyo atasomewa leo iwapo mfumo wa usajili kimtandao utakubali.

Tukio lilivyotokea

Tukio la mwanafunzi Alex kumjeruhi mwalimu wake Stanford Mgaya kwa kumkata panga kichwani na mkono lilitokea Sepetemba 25, 2023 wakati mwalimu huyo akiwa ofisini akitekeleza majukumu yake.

Kabla ya kumshambulia wake, mwanafunzi huyo anadaiwa kuingia ofisini na kumwelza kuwa alienda ili wamalizane kuhusu adhabu aliyopewa yeye na wenzake wengine 16 kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Baada ya shambulio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa aliimbia Mwananchi kuwa mwanafunzi huyo anashikiliwa kwa uchunguzi kabla ya kumfikishwa mahakamani.

Tangu wakati huo, Jeshi la Polisi limeendelea kumshikilia Alex hadi jana alipofikishwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashtaka kabla ya kurejeshwa mahabusu ya polisi baada ya mfumo wa usajili kugoma.

Hali ya mwalimu

Hali ya kiafya ya mwalimu Mgaya aliyelazwa Hospitali Teule Wilaya ya Sengerema imeimarika na tayari alisharuhusiwa kurejea nyumbani tangu Septemba 27, mwaka huu.

Chanzo: mwanachidigital