Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mstaafu jela au faini ya Sh1 milioni kwa kutoa rushwa

HUKUMU Mstaafu jela au faini ya Sh1 milioni kwa kutoa rushwa

Fri, 1 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tabora. Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemuhukumu, Jesca Yegera (60) kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa Sh1milioni baada ya kupatikana na hatia ya kumpa rushwa Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Sh500,000 ili alipwe madai ya malimbikizo ya mshahara wke wa miezi mitano ambayo ni zaidi ya Sh6 milioni.

Adhabu hiyo imetolewa leo Alhamisi Novemba 30, 2023 na Hakimu Edda Kahindi baada ya mshtakiwa ambaye ni mtumishi mstaafu kupatikana na hatia ya makosa mawili ya kushawishi na kutoa rushwa hiyo.

Awali Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Igunga, Mazengo Joseph aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo Juni 24, 2022.

Ameieleza Mahakama kuwa tarehe hiyo mchana akiwa kwenye ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, mshtakiwa alimshawishi kumpatia rushwa ya Sh500,000 kwa njia ya simu Ofisa Utumishi Mwandamizi, Erick Sije (38) anayefanya kazi katika Halmashauri ya wilaya ya Igunga.

Mazengo ameiambia Mahakama kuwa mshtakiwa huyo alishawishi na kutoa rushwa ya Sh300,000 kati ya Sh500,000 alizoahidi kwa njia ya simu ili aweze kumsaidia kupata madai yake ya malimbikizo ya mshahara wa miezi mitano ya zaidi ya Sh6 milioni aliyokuwa akidai.

Amesema mshtakiwa huyo ametenda makosa hayo mawili kinyume na kifungu cha 15 (1) (b) (2) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa sura 329 mapitio ya 2019 inayozuia kutenda makosa kama hayo.

Hata hivyo baada ya kusomewa mashtaka hayo mawili, mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo mawili na ndipo upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi sita mahakamani ambao walitoa ushahidi huku upande wa mshtakiwa akiwa shahidi yeye na mume wake.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili,Hakimu Edda Kahindi amesema pasipo shaka yoyote kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri umemuona mshtakiwa Jesca Yegela ana hatia.

Amesema Mahakama inamhukumu kulipa faini ya Sh1 milioni na akishindwa kulipa atakwenda jela miaka mitatu ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live