Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msimamizi mkuu wa ustawi wa jamii Dar jela miaka mitatu

25089 KIFUNGO+PIC TanzaniaWeb

Fri, 2 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Msimamizi mkuu wa ustawi wa jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Deogratus Shirima amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kukutwa na hatia ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh200,000 kutoka kwa Hamadi Juma.

Hukumu hiyo imetolewa leo Alhamisi Novemba Mosi, 2018 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Caroline Kiliwa.

Ni baada ya kukutwa na makosa mawili; kupokea rushwa ambalo adhabu yake kifungo cha miaka miwili jela na kuomba rushwa ambalo kifungo chake ni mwaka moja, kufanya jumla ya miaka kuwa mitatu.

Akisoma hati ya mashtaka,  mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Stella Mafuru amedai  Mei 11, 2017 mshtakiwa aliomba rushwa ya Sh200,000 kwa Juma huku akijua kufanya hivyo ni kosa.

Katika shtaka la pili amedai Mei 16, 2017 mshtakiwa alipokea rushwa ya Sh200,000 kutoka kwa Juma huku akijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Hukumu hiyo ilitakiwa isomwe juzi lakini mshtakiwa huyo alikiuka dhamana na kulazimika upande wa mashtaka kumtafuta na kumkamata.

Ilivyokuwa

Hakimu: Ulikuwa wapi jana huku ukijua una kesi mahakamani.

Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu jana nilikuwa naumwa nilienda kutibiwa.

Hakimu: Dhamana inasemaje unapoumwa? Unatakiwa utibiwe hospitali gani na huo utaratibu wa kwenda katika hospitali binafsi wakati unatakiwa utibiwe katika hospitali za Serikali,  je unafahamu hilo?

Mshitakiwa: Sifahamu

Hakimu: Wakati unapigiwa simu na mdhamini wako kwa nini ulidanganya upo Dodoma na ulipoongea na mimi uliniambia unaumwa upo hospitalini.

Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu jana nilitoa taarifa kuwa ninaumwa.

Hakimu:  Wakati unaongea na wadhamini wako simu iliwekwa loud speaker kila kitu ulichokuwa unazungumza kilisikika, kwanza ulimwambia mdhamini wako upo njiani unaelekea Dodoma lakini mdhamini wa pili ulimwambia upo hospitali unaumwa na mimi nilipokuuliza ukaniambia upo hospitali je huoni kama ulikuwa unaidanganya mahakama?  

Baada ya mahojiano hayo, hakimu amesema mshtakiwa ametiwa hatiani kwa makosa mawili na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz