Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa iwapo mtumishi wa umma, Jonas Afumwisye anayedaiwa kufutwa kazi katika Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kumkashifu Rais Samia Suluhu kwenye mitandao ya kijamii, anapaswa kukataa rufaa kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa Umma.
Afumwisye ambaye alikuwa Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam wa TRC alifutwa kazi hivi karibuni huku wananchi wengi wakihoji juu ya hatua hiyo kuwa inaminya uhuru kwa watumishi wa umma.
Mapema jana Msemaji Mkuu wa Serikali , Gerson Msigwa ameieleza kuwa hana taarifa rasmi za kufutwa kazi kwa mtumishi huyo aliyekuwa akihudumu kama Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam.
”Sina taarifa za kufutwa kazi lakini alifanya kosa kwa mujibu wa sheria za utumishi basi atakuwa amechukuliwa hatua. Mtumishi wa umma naye ana haki ya kukata rufaa pale anapoadhibiwa…
”…suala kama hili si kwa yeye tu, watumishi wengi wa umma wana mashauri, wengine kufukuzwa ikibainika walitenda kosa lakini wana haki ya kusikilizwa na kujitetea,” alisema Msigwa.
Mtumishi huyo alidaiwa kueleza kutoridhishwa na kupanda kwa tozo kwenye miamala ya kielektroniki jambo ambalo Serikali imekana kuwa ilikuwa ndio sababu ya kufukuzwa kwake.
Msigwa alisema, ”Siwezi kusema kufutwa kwake kazi kuna tokana na yeye kuzungumzia kuongezeka kwa tozo za miamala ya kielektroniki. Huenda sababu ni zingine.”
Ilipoanzishwa tozo ya miamala ya simu Julai 15 mwaka jana, kampuni za simu ziliungana na wananchi kuilalamikia huku benki kadhaa zikiwataka wananchi kutumia huduma zao kwamba ni nafuu zisizo na makato mengi. Mwaka huu Serikali ikaongeza tozo kwa upande wa mabenki na kuacha wananchi wakilalamika.