Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msichana wa kazi anayedaiwa kuiba mtoto wa siku moja adakwa

65237 Pic+msichana

Tue, 2 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Msichana Christina Claudia (23) mfanyakazi wa ndani anashikiliwa na polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za kuiba mtoto wa kiume wa mwaka mmoja wilayani Kilosa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Julai 2, 2019 Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea Juni 25, 2019 majira ya saa 3 asubuhi huko kitongoji cha Manzese A kata ya Mkwatani wilayani Kilosa.

Amesema msichana huyo anadaiwa kumdanganya Mariet Deogratius (16) ambaye ni dada wa mtoto huyo (Thomas Deogratius mwenye mwaka mmoja) aliyeibiwa kuwa anaenda naye kufua nguo bombani ndipo alipopata mwanya wa kumtorosha kisha kutoweka na mtoto huyo.

Kamanda huyo amesema mama wa mtoto huyo Flora Thomas (32) alikuwa kazini na ilipofika muda wa saa 6 mchana aliagiza mtoto wake apelekewe anakofanyia kazi ili aweze kumnyonyesha kwani amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara ndipo aliambiwa mtoto huyo alitoka na dada huyo wa kazi wa jirani yake.

Mutafungwa amesema baada ya kukaa muda mrefu bila msichana huyo kurudi ndipo walipoamua kutoa taarifa kituo cha  polisi Kilosa na kuanza kufutilia.

Amesema walifanikiwa kumkamata dada huyo wa kazi  Juni 29, 2019, katika kijiji cha Mwakabasa, kata ya Mahonda wilaya Nzega mkoani Tabora akiwa na mtoto huyo.

Pia Soma

Kamanda huyo amesema mtoto huyo tayari amekabidhiwa kwa wazazi wake akiwa salama na kwa sasa anafanyiwa uchunguzi wa kiafya kubaini kama amepatwa na madhara yoyote.

Kamanda huyo alisema msichana huyo wa kazi anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi na kufahamu alikuwa na nia gani kwa mtoto huyo na kwamba atafikishwa mahakamani wakati wowote mara baada  ya uchunguzi kukamilika.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa mtoto wake, Frola Thoms amesema anamtambua msichana Christine kama dada wa kazi wa mmoja wa wapangaji wake na wamekuwa wakiishi pamoja kwa muda mrefu.

“Kama mzazi lazima uchanganyikiwe kwani kumpoteza mtoto si jambo la mzaha, nimekuwa nikisikia watoto wanapotea kwenye maeneo mengi lakini sasa limenikuta mimi nilikuwa na huzuni lakini wakati huo nikawa na imani kuwa atapatikana kwa msaada wa polisi,” amesema

Chanzo: mwananchi.co.tz