Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msichana aliyeuawa chumbani kuagwa leo Dar

F9aceab6d26a35ded6091418679c3497 Msichana aliyeuawa chumbani kuagwa leo Dar

Fri, 22 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MWILI wa Belinda Carlos (19) anayedaiwa kuuawa nyumbani kwao, Goba Tegeta A, Dar es Salaam unatarajiwa kuagwa leo katika Hospitali ya Mloganzila, na kisha kusafirishwa kwenda mkoani Iringa kwa maziko.

Mama wa kambo wa marehemu, Pendo Carlos anatuhumiwa kumuua Belinda Januari 19 asubuhi na akawatumbukiza shimoni wanawe wawili Bryton Carlos (6) na Bertha Carlos (4).

Hali za watoto hao waliotumbukizwa kwenye shimo linalodaiwa kutumika kukinga maji ya mvua lenye urefu wa futi 20 zinaendelea vizuri.

Inadaiwa kuwa baada ya Pendo kumuua Belinda alikwenda gesti kwa lengo la kujiua lakini yupo hai hospitalini jijini Dar es Salaam.

Binamu wa marehemu, Jonathan Adam alisema jana kuwa mwili wa Belinda umehifadhiwa Hospitalini Mloganzila na kwamba msiba upo kwa shangazi yake Mbezi Marambamawili.

"Ilikuwa tusafirishe leo (jana) lakini tumeambiwa tuache mwili ili uchunguzwe zaidi," alisema Jonathan.

Alieleza kuwa, siku ya tukio alikuwa safarini Mbinga na alipigiwa simu kupewa taarifa hiyo.

Jonathan alisema wakati anaondoka nyumbani kusafiri nyumbani kulikuwa na amani na hakuna yeyote aliyekuwa amegombana na mama huyo anayedaiwa kumuua Belinda.

Mjumbe wa shina la Tegeta A, kata ya Goba, Juma Issa alisema alipigiwa simu na wananchi kuhusu mama huyo kutenda tukio hilo na alipofika walikuta mwili wa Belinda ukiwa umelala ndani na pembeni kukiwa na mtandio.

"Ilikuwa majira ya asubuhi saa 2:00 Jumanne tarehe 19, kabla ya mauti binti huyo alionekana akitoka dukani akiwa amebeba mkate kwa ajili ya maadalizi ya kifungua kinywa," alisema.

Issa alisema jambo la ajabu baada ya kutenda kitendo hicho mtuhumiwa alipiga simu na ndiyo maana hata watoto wake walijulikana walipodumbukizwa shimoni la kisima ambacho hakikufunikwa na maji hayakuwa mengi.

Alisema hajawahi kupata malalamiko yoyote kutoka kwa mtuhumiwa na kwamba ni mama aliyekuwa amechangamka akifanya kazi zake hata baada ya mume wake kufariki dunia mwaka jana.

Mwanasaikolojia, John Ambrose jana alilieleza gazeti hili kuwa, kwa kawaida mwanadamu ana sehemu tatu ambazo ni fikra, hisia na vitendo.

Alisema kutokana na matukio mwanadamu huingiwa na fikra kuhusu suala husika kisha hukaribisha hisia kutokana na suala hilo na ndipo kitendo kinafuata.

Ambrose alisema kama mtu asipojiwahi au kuwahiwa huenda akafanya jambo baya na ndio maana watu wa aina hiyo huchukua uamuzi wa kufanya mambo ambayo yanakuwa ni suluhisho la muda mfupi au linaloweza kuwa na madhara kwake au kwa jamii.

Alisema uamuzi wa kujiua huweza kuwa kati ya suluhisho la mhusika anayepitia changamoto mbaya au wengine huchukua uamuzi wa kuua mtu au watu wanaomkwaza au wengine kuamua kuua na kujiua.

Alisema kama mtu huyo asipopata ushauri mzuri unaoweza kumfariji na kuendelea kulundika machungu muda mrefu huruhusu roho ya ukatili kumuingia na huweza kusababisha maafa.

Mtaalamu wa Afya ya Akili, Dk Aisack Lema alisema jamii inatakiwa kufundishwa elimu ya utambuzi wa matatizo ambayo itawasaidia kukabiliana na matatizo bila ya kujiua.

Alisema kuna faida kubwa kutatua tatizo bila ya mhusika kujidhuru au kusababisha madhara kwa watu wengine kwa kuwa aliye na elimu hiyo atakuwa na uwezo wa kumudu hisia hasa zinazomtaka kufanya mabaya.

Chanzo: habarileo.co.tz