Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msichana ajinyonga chooni akituhumiwa kuiba 5,000/-

Bdaf5f8ddfa37d825004d7f2c6b59b8b.jpeg Msichana ajinyonga chooni akituhumiwa kuiba 5,000/-

Thu, 27 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATU wawili Pwani wamekufa katika matukio mkoani Pwani likiwemo la mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 14 aliyepoteza maisha kwa kujinyonga baada ya mama yake kumtuhumu kuiba Sh 5,000.

Msichana huyo ambaye jina lake limehifadhiwa, alikuwa akisoma Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Mtongani, Mlandizi wilayani Kibaha.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Wankyo Nyigesa alisema jana kuwa mwanafunzi huyo alikutwa amejinyonga ndani ya choo cha nyumbani kwao.

Aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kuwa tukio hilo lilitokea Mei 22, mwaka huu huko katika Mtaa wa Shule ya Msingi Mtongani kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

“Chanzo cha kifo hicho ni mama yake kumtuhumu kuiba fedha hizo na kuchukua maamuzi hayo ya kujinyonga hadi kufa ambapo mama mzazi wa mtoto huyo Ashura Seleman na baba yake mlezi wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi ili kujua undani wa tukio hilo,” alisema Kamanda Nyigesa.

Alisema katika tukio lingine, Mrisho Omary maarufu kwa jina la Shomvi anayeishi Mtaa wa Umwelani katika Kata ya Kongowe wilayani Kibaha, amefariki dunia na watu wengine wawili wamejeruhiwa baada ya nyumba walimokuwa wamelala kuchomwa moto na watu wasiojulikana kwa madai kuwa ni wezi.

Alisema watu hao walikuwa wamelala kwenye nyumba ya udongo iliyoezekwa kwa nyasi mali ya Omary Kapite.

Alisema tukio hilo lilitokea Mei 15, mwaka huu saa 5:00 usiku katika Mtaa wa Umwelani katika Kata ya Kongowe na kwamba Omary alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi.

Kamanda Nyigesa alisema watu hao baada ya kutuhumiwa ni wezi, nyumba ilichomwa moto na kuwasababishia majeraha na na hatimaye kifo cha Omary Mei 17, mwaka huu.

“Upelelezi wa awali umebaini kuwa kulikuwa na ugomvi wa kimapenzi baina ya Zuwena Mahira na watu hao na upelelezi bado unaendelea juu ya tukio hilo ili kuwabiani waliohusika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao,” alisema Kamanda Nyigesa.

Alisema wananchi waliichoma moto nyumba baada ya Zuwena kupiga kelele kuwa watu hao walitaka kumbaka na kumwibia Sh 30,000 na simu.

“Baada ya watu kusikia zile kelele walikwenda na kuanza kuwakimbiza ambapo waliingia kwenye nyumba hiyo na kujichukulia sheria mkononi kwa kuichoma moto nyumba hiyo na kuwasababishia watu hao majeraha na marehemu baada ya siku mbili alifariki dunia,” alisema.

Katika tukio lingine, Polisi imewakamata watu 84 kwa tuhuma za kukutwa na vitu mbalimbali wakati wa operesheni kati ya Mei 9 hadi 25, mwaka huu.

Kamanda Nyigesa alisema walifanya operesheni hizo ni kudhibiti makosa ya jinai na makosa ya usalama barabarani.

Alitaja baadhi ya vitu vilivyokamatwa kuwa ni mifuko miwili ya bangi, puli 17 na kete 536, noti 24 za nchi za China, Philipino, Vietnam na Msumbiji, pikipiki tano na mifuko 20 ya maziwa ya unga.

Chanzo: www.habarileo.co.tz