Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshtuko ghala la pembe za ndovu

Pembe Web Mshtuko ghala la pembe za ndovu

Tue, 11 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mali bila daftari huisha bila habari! Ni msemo wenye maana kwamba ni vyema kuweka kumbukumbu za vitu vyako katika mahali pa usalama na katika mpangilio mzuri au kupangilia kazi zako kwa ufasaha zaidi ili kukuwezesha kujua, kutambua kwa urahisi mwenendo mzuri wa kazi zako.

Wakati kukiwa na angalizo hilo la wahenga, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini tatizo katika utunzaji wa taarifa za pembe za ndovu kwenye ghala la serikali.

Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/22 iliyowasilishwa bungeni jijini hapa wiki iliyopita, CAG Charles Kichere, amebaini kuwa moto uliodaiwa kuteketeza ghala la pembe za ndovu mwaka 2013, haukuchunguzwa.

CAG Kichere alisema alibaini kuwa mwaka 2013 kulikuwa na tukio la moto kwenye ghala la pembe za ndovu ambalo lilisababisha kupotea kwa taarifa muhimu zinazohusiana na pembe za ndovu zilizohifadhiwa.

“Jambo la kushangaza ni kuwa hakuna uchunguzi uliofanyika ili kubaini chanzo cha moto huo na madhara yake hadi wakati wa ukaguzi.

"Nilibaini kutopatikana kwa taarifa sahihi za pembe za ndovu zilizohifadhiwa kwa ajili ya kufanya tathmini na kuzipima upya pembe hizo za ndovu, hali isiyoridhisha ya pembe zote zilizohifadhiwa kiasi cha kusababisha kuharibika kwa ubora na hadhi yake na kushindwa kuhuisha rejista juu ya hali na thamani za pembe za ndovu," anabainisha.

CAG pia anasema amebaini programu iliyotumika kurekodi na kusajili akiba ya pembe za ndovu na nyara zingine haijaunganishwa na seva kuu ya programu ya wizara kwa sababu programu hiyo ilikuwa imepitwa na wakati, baadhi ya pembe za ndovu zilikosa taarifa zake za maandishi, huku nyingine zikiwa na taarifa zisizosomeka kutokana na ubovu wa paa la kuhifadhia uliosababisha kuvuja kwa paa hilo.

Anataja kasoro zingine zinajumuisha zana za kuwekea alama zilizotumiwa kurekodi taarifa juu ya pembe za ndovu ziliandikwa kwa wino unaoweza kufutika, na kuzifanya zifutike kwa urahisi na ghala la kuhifadhia lilikuwa katika hali mbaya kutokana na kuwa na nafasi ndogo, paa kuvuja, hewa chafu, mazingira machafu, umeme usio imara, ukosefu wa kamera na vifaa vya kuzima moto.

"Kwa maoni yangu, ukosefu wa udhibiti sahihi wa pembe za ndovu unaweza kusababisha upotevu wa taarifa zinazohusiana na pembe za ndovu, taarifa hizi ni muhimu katika kesi za kisheria dhidi ya ujangili na juhudi nyingine zinazolenga kudhibiti vitendo vya ujangili,” CAG anatoa angalizo.

Anabainisha kuwa Menejimenti ya Wizara imethibitisha kuwapo upungufu huo na itafanya uhakiki wa nyara kila baada ya miaka mitatu hadi minne, kulingana na upatikanaji wa rasilimali.

"Napendekeza Wizara ya Maliasili na Utalii iweke mfumo madhubuti wa kudhibiti na kusimamia pembe za ndovu.

"Pia, iandae mfumo madhubuti wa kuhifadhi kumbukumbu za taarifa zote zinazohusiana na pembe za ndovu, ukiwamo mpango mkakati wa taarifa za upotevu kutokana na matukio yasiyotarajiwa kama vile moto," CAG anawasilisha hoja yake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live