Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshtakiwa mwingine kesi ya Nida, amwandikia barua DPP

Mshtakiwa mwingine kesi ya Nida, amwandikia barua DPP

Tue, 29 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mshtakiwa katika kesi ya Uhujumu Uchumi, Xavery Silverius, ameandika barua ya kukiri na kuomba msamaha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Kayombo na wenzake wanne akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nchini Tanzania (Nida), Dickson Maimu wanakabiliwa na mashtaka 55 likiwamo la kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.175 bilioni.

Hayo yameelezwa jana Oktoba 28, 2019 na wakili wake, Tully Kaundime mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally wakati Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 7/2019 ilipotajwa.

Tully alisema mteja wake aliandika barua hiyo Septemba 26, 2019 lakini mpaka jana alikuwa bado hawajapata majibu kuhusiana na maombi hayo.

Kutokana na hali hiyo, aliomba upande wa mashtaka ueleze umefikia hatua gani baada ya mteja wake kuwasilisha barua kwa DPP.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya aliiambia mahakama  kuwa kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na kubadilisha hati ya mashtaka.

Pia Soma

Advertisement

Katika hati hiyo mpya ya mashtaka, wamemuondoa mshtakiwa Astery Ndege ambaye alikiri mashtaka yake na kuamriwa na mahakama hiyo kurejesha Serikalini Sh293,446,400.23.

Ndege ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers anarejesha kiasi hicho cha fedha ikiwa ni sehemu ya hasara iliyosababishwa na washtakiwa hao ya Sh1.175 bilioni.

Kwa sasa hati hiyo mpya, ina mashtaka 55 badala ya 100 yaliyokuwapo awali.

Hakimu Ally baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 11, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali (PH).

Mbali na Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Avelin Momburi, George Ntalima, Xavery Silverius maarufu kama Silverius Kayombo na Sabrina Raymond.

Hata hivyo, Maimu, Ntalima na Silverius wamerudishwa rumande kutokana na kuwa na mashtaka ya kutakatisha fedha ambayo hayana dhamana, huku Momburi na Raymond wakiwa nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba Mahakaka Kuu.

Katika mashtaka hayo 55, yapo ya kuongoza genge la uhalifu, kutakatisha fedha, kughushi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.175 bilioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz