Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshtakiwa kesi ya kughushi saini ya Makamba kuhojiwa Takukuru

31632 Nemcpic TanzaniaWeb

Fri, 14 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam,  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeruhusu,Magori Wambura mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari  Makamba,  kwenda kuhojiwa na Takukuru.

Wambura ambaye ni ofisa mazingira  kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kula njama na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Desemba 14, 2018 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando baada ya upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo  kumhoji mshtakiwa huyo.

Wakili kutoka Takukuru, Leonard Swai ameieleza mahakama hiyo kuwa wanaomba kibali cha kumhoji mshtakiwa huyo kwa makosa mengine.

Baada ya Swai kutoa maelezo hayo, Hakimu Mmbando alikubaliana na upande wa mashtaka na kuruhusu Wambura kwenda kuhojiwa.

"Mahakama imekubali Wambura ahojiwe lakini wakati anahojiwa wakili wake anaruhusiwa kushiriki katika mahojiano hayo,” amesema hakimu Mmbando.

Hakimu Mmbando baada ya kueleza hayo ameahirisha  kesi hadi Desemba 19, 2018 itakapotajwa.

Wambura anatetewa na wakili Ntumika Godfrey na yupo  rumande katika gereza la Segerea baada ya kukosa dhamana.

Awali,  kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Mbali na Wambura washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ambao ni wafanyakazi wa  NEMC ni ofisa mazingira, Deusdith Katwale(38),   mtaalam wa Tehama, Luciana Lawi(33), katibu muhtasi, Edna Lutanjuka (51).

Wengine ni  maofisa wawili wasaidizi wa mazingira , Mwaruka Mwaruka (42) na  Lilian Laizer (27) wote  wakazi wa Ukonga Mombasa.

Mbali na kughushi, washtakiwa hao  wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kuwasilisha nyaraka za uongo na  kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya Sh160milioni.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Kisutu,  Oktoba 31, 2018 na kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Washtakiwa watano wako nje kwa dhamana isipokuwa Wambura ambae anaendelea kusota rumande baada ya kukosa dhamana.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa  kati ya Septemba 27, 2016 na April Mosi, 2018 jijini Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kughushi.

Soma zaidi: Watumishi watano Nemc mahakamani, wadaiwa kughushi saini ya Waziri Makamba



Chanzo: mwananchi.co.tz