Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshtakiwa kesi ya kughushi saini ya Makamba aruhusiwa kusafiri

32490 Pic+makamba Tanzania Web Photo

Wed, 19 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia mshtakiwa Edna Lutanjuka, mfanyakazi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) kwenda wilayani Bukoba mkoani Kagera kama alivyoomba.

Edna na wenzake watano ambao wote ni wafanyakazi wa baraza hilo  wanakabiliwa na kesi ya kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba.

Mbali na kughushi, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mengine yakiwemo ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya Sh160 milioni.

Leo Jumatano Desemba 19, 2018 wakili wa Serikali, Jenipher Masue amedai mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Augustina Mmbando  kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili kutajwa na kuongeza kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Baada ya kueleza hayo, mshtakiwa Edna alinyoosha mkono na kuiomba mahakama hiyo impe kibali cha kwenda Bukoba .

Hakimu Mmbando baada ya kusikiliza maombi hayo alimruhusu mshtakiwa kusafiri kwenda na kumtaka afike bila kukosa kesi hiyo itakapotajwa tena. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 3, 2019.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni ofisa wa mazingira Nemc, Deusdith Katwale (38) na mtaalam wa Tehama wa baraza hilo, Luciana Lawi (33) wote wakazi wa Ubungo Msewe.

Wengine ni  ofisa mazingira Magori Wambura (38) mkazi wa Bombambili, katibu muhtasi wa baraza hilo, Edna Lutanjuka (51) mkazi wa Mbezi Beach St Gasper, msaidizi wa ofisi, Mwaruka Mwaruka (42) na ofisa mazingira wa Nemc, Lilian Laizer (27) wote  wakazi wa Ukonga Mombasa.

Wafanyakazi hao walifikishwa mahakamani Oktoba 31, 2018 na kusomewa mashtaka sita ya uhujumu uchumi, ikiwemo kughushi saini ya Makamba katika vyeti vya tathmini ya uharibifu wa mazingira.

Katika kesi hiyo washtakiwa watano wako nje kwa dhamana isipokuwa mshtakiwa namba moja, Wambura anayesota rumande baada ya kukosa dhamana.



Chanzo: mwananchi.co.tz