Dar es Salaam. Astery Ndege, mshtakiwa wa tatu katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili na wenzake watano akiwemo aliyekuwa mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kurejesha serikalini Sh293.4 milioni.
Ndege ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers anarejesha kiasi hicho cha fedha ikiwa ni sehemu ya hasara iliyosababishwa na washtakiwa hao ya Sh1.175 bilioni.
Akitoa hukumu hiyo leo Jumanne Oktoba 8, 2019 Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally amesema mshtakiwa huyo atalipa fedha hizo kwa mujibu wa makubaliano kama sehemu ya fidia ya hasara aliyoisababisha.
Mbali na adhabu hiyo, Hakimu Ally ameamuru mshtakiwa Ndege kulipa faini ya Sh4 milioni na akishindwa atatumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Amesema ametoa hukumu hiyo baada ya kuzingatia kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa kwanza, amekiri akiashiria kujutia kosa lake.
Wakili wa Serikali mwandamizi, Ladslaus Komanya amesema hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshtakiwa huyo, kwamba ni mkosaji kwa mara ya kwanza.
Pia Soma
- Auawa na polisi akidaiwa kutaka kuiba vifaa vya ujenzi
- Majaliwa kuupokea mwenge Ruangwa
- Vikwazo 175 visivyo vya ushuru vyapatiwa ufumbuzi EAC.
Pia imesaidia katika kampeni ya kupunguza msongamano wa wafungwa gerezani.
Wakili wa mshtakiwa huyo, Godwin Nyaisa aliungana na upande wa mashtaka kuwa mshtakiwa ni mkosaji kwa mara ya kwanza na amekaa mahabusu kwa miezi 10, “ameonja ladha ya gereza, mahakama itoe adhabu ya faini.”
Ndege ambaye ni mshtakiwa wa tatu kati ya washtakiwa sita ataanza kulipa Sh50 milioni kwa awamu ya kwanza.
Awali, kabla ya kusomwa kwa barua yake ya kukiri makosa, wakili Komanya aliwasomea mashtaka mapya washtakiwa hao ambayo yalipungua kutoka 100 ya awali hadi 50.
Wakati wa usomwaji wa mashtaka hayo Maimu na wenzake watano waliyakana mashtaka yote lakini Ndege alikiri na kusomewa maelezo ya awali, kisha akatiwa hatiani na kuhukumiwa.
Miongoni mwa mashtaka yanayomkabili Maimu na wenzake wanne ni kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.175 bilioni.
Mengine ni utakatishaji fedha, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo ili kumdanganya mwajiri wao na kuisababishia mamlaka hiyo hasara, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Mbali na Maimu washtakiwa wengine ni meneja biashara wa Nida, Aveln Momburi; ofisa usafirishaji, George Ntalima; mkurugenzi wa sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.
Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na Oktoba 15, 2019 itatolewa tarehe ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.