Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshtakiwa kesi ya Maimu afariki dunia

Fri, 19 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.  Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepokea hati ya kifo ya mshtakiwa wa tatu, Benjamin Mwakatumbula aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Mwakatumbula na wenzake saba akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida)  Dickson Maimu, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.16 bilioni.

Mwakatumbula wakati wa uhai wake alikuwa kaimu mhasibu mkuu wa Nida.

Taarifa ya hati ya kifo chake imewasilishwa leo Jumanne Oktoba 16, 2018 na upande wa utetezi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri  wakati kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),  Imani Mitumizizi amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na wakili anasimamia shauri hilo, amesafiri kwenda Musoma.

"Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika hivyo tunaomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai wakili Matumizizi.

Hata hivyo,  kabla ya kuendelea kwa kesi hiyo, mshtakiwa Maimu alimkabidhi wakili wa utetezi,  Faisal Ali bahasha ya kaki na ilipofunguliwa ilikuwa na hati ya kifo na kuikabidhi upande wa mashtaka.

Mitumizi baada ya kuipitia hati hiyo alimpatia hakimu Mashauri ili nae aweze kuikagua.

Hakimu Mashauri baada ya kuikagua hati hiyo amesema Mahakama imepokea hati ya kifo cha Mwakatumbula na mwenendo wa kesi dhidi yake umefutwa.

"Mahakama imepokea hati ya kifo cha Mwakatumbula na mwenendo wa kesi dhidi yake umefutwa kuanzia leo," amesema Hakimu Mashauri.

Hakimu Mashauri baada ya kueleza hayo ameahirisha kesi hiyo hadi  Novemba 15, 2018.

Mbali ya Maimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni meneja biashara wa Nida, Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani.

Wengine ni  mkurugenzi wa kampuni ya Aste Insurance Brokers,  Astery Ndege;  Ofisa Usafirishaji,  George Ntalima;  Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka ya kutumia madaraka vibaya, kula njama, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh1.169 bilioni

 

Chanzo: mwananchi.co.tz