Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshtakiwa aomba kadi ya benki mahakamani, hakimu aweka msisitizo

82585 Pic+karugendo Mshtakiwa aomba kadi ya benki mahakamani, hakimu aweka msisitizo

Sat, 2 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Aliyekuwa mkurugenzi wa uthaminishaji almasi na vito Tanzania, Archard Kalugendo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa hajapewa kadi yake ya benki ili aweze kutoa maelekezo ya kutoa fedha kwa ajili ya familia yake licha ya kuomba suala hilo kwa muda mrefu.

Kalugendo ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.4 bilioni.

Julai 12, 2019 mshtakiwa huyo aliiomba mahakama hiyo imsaidie  aweze kupewa kadi hiyo baada ya kumwandika barua mkurugenzi wa mashtaka ( DPP).

Mbali na Kalugendo, mshtakiwa mwingine ni aliyekuwa mthamini wa madini hayo wa Serikali, Edward Rweyemamu ambao wote wapo rumande kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Leo Ijumaa Novemba Mosi, 2019 Kalugendo amewasilisha tena ombi hilo mahakamani hapo  baada ya kuulizwa na

Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shaidi kama ameshapatiwa kadi hiyo. Mpaka sasa tunavyozungumza  bado sijapatiwa kadi yangu ya benki tangu nilipoandika barua kwa DPP,” amesema mshtakiwa huyo.

Baada ya kuieleza hayo, Hakimu Shaidi ameutaka upande wa mashtaka kupitia kwa mkuu wa waendesha mashtaka katika Mahakama ya Kisutu kufuatilia maombi hayo ili washtakiwa wapewe kadi zao.

" Nataka Wankyo (wakili wa Serikali mwandamizi) ashughulikie suala hili kwa sababu mshahara si unajulikana ni kiasi fulani kinaingia katika akaunti,” amesema hakimu.

Hakimu Shaidi   ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kesi inayowakabili  kutokuwa na dhamana.

Awali, Wakili wa Serikali Daisy Makakala amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na jalada linafanyiwa kazi na DPP.

Kalugendo na Rweyemamu wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 54/2017.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali  Dar es Salaam na Shinyanga.

Kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathaminishaji wa almasi wa Serikali na waajiriwa wa Wizara ya Nishati na Madini waliisababishia Serikali hasara ya Dola  1,118,291.43 za Marekani sawa na Sh2.4 bilioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz