Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshtakiwa akiri kutumia jina la Rais Samia Facebook

Kotini Samia Pic Data Mshtakiwa akiri kutumia jina la Rais Samia Facebook

Fri, 2 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Mkazi wa Mwanza, Nickson Mfoi (20) amekiri kutumia jina la Rais Samia Suluhu Hassan katika akaunti yake ya Facebook, kinyume cha sheria na kwamba kupitia akaunti hiyo, ameweza kujipatia Sh40, 000.

Mfoi amekiri jana, Septemba Mosi, 2022 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati akisomewa maelezo ya awali (PH), baada ya upelelezi wa kesi yake kukamilika.

Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujitambulisha kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika mtandao wake wa kijamiia wa Facebook, wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Akisomewa maelezo yake na  wakili wa Serikali Ashura Mnzava , amedai Septemba, 22, 2021 mshitakiwa  akiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia ya kulaghai Umma, alijiwasilisha kama Rais Samia Suluhu Hassan katika mtandao wa kijamii, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Amedai mshitakiwa katika jina la akaunti yake ya Facebook aliandika Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo alijipatia fedha kupitia mtandao huo wa kijamii.

Wakili Mnzava amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate kuwa, Oktoba 2, 2021 mshtakiwa akiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anadaiwa kukutwa akitumia laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na Getness Jackson bila kuisajili kwa kutumia alama ya vidole au kutoa taarifa kwa mtoa huduma.

Mahakama iliendelea kuelezwa kuwa mshitakiwa alikamatwa katika hoteli ya Malaika, iliyopo mkoani Mwanza na alipofanyiwa upekuzi na askari alikutwa akimiliki simu moja aina Infinix na laini iliyosajiliwa kwa jina la Jackson na kisha kukamatwa.

Mnzava amedai wakati anahojiwa kituoni na askari polisi alikiri kutenda makosa hayo na Agosti 4, 2022 na alifikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.

Alidai wakati anahojiwa na askari alikiri kutenda makosa hayo na Agosti 4, 2022 alifikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.

Mshtakiwa baada ya kusomewa maelezo yake, alikiri maelezo yake, majina yake na pia kuwa yeye ni mkazi wa mkoani Mwanza na kwamba akaunti hiyo ya Facebook aliuziwa na mtu.

Kutokana na kukiri maelezo yake, Hakimu Kabate akataka kujua ni kiasi gani alichokipata kupitia akauniti hiyo ya facebook yenye jina la Rais?  Mshtakiwa amejibu kuwa alipata Sh 40,000.

Hakimu Kabate baada ya kusikiliza maelezo hayo, amesema kwa kuwa mshtakiwa amekiri kuwa alikuwa anatumia laini ya simu na akaunti hiyo, ni vyema upande wa mashtaka wakawasilisha vielelelezo hivyo mahakamani Septemba 7, 2022.

Baada ya kusema hayo, Hakimu Kabate ameahirisha kesi hadi tarehe hiyo ambapo kesi hiyo itaendelea.

Mshitakiwa amerudishwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Chanzo: Mwananchi