Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshtakiwa akana mashtaka aliyoyakubali awali

20315 NMB+pic TanzaniaWeb

Tue, 2 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo wilaya ya Kinondoni imeshindwa kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa watatu wanaokabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la wizi wa simu 17 mali ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Hali hiyo ilitokana na mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo, kukana mashtaka yanayomkabili.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni mlinzi wa TCRA, Rashid Abdallah, Fatuma Rajabu na Idd Bago,  wote wakazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam.

Septemba 17, 2018 walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka yanayowakabili, mshtakiwa wa tatu ambaye ni Bago alikiri mashtaka hayo, na mahakama hiyo kupanga kuendelea na kesi hiyo leo Jumatatu Oktoba Mosi, 2018.

Leo Bago amebadili ‘gia angani’ kwa kukana mashtaka hayo na mahakama kulazimika kuahirisha shauri hilo hadi Oktoba 8, 2018.

Awali,  kabla ya kuwasomea maelezo ya awali, mwendesha mashtaka, Januari Kosekwa ameieleza mahakama kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kuwasomea mashtaka washtakiwa hao.

Kosekwa amedai washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la wizi wa simu 17 mali ya TCRA.

Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Januari 9, 2018 saa sita mchana katika ofisi zilizopo wilaya ya Kinondoni  waliiba simu 17 aina ya KZG mobile phone 6 Dougeex51,Tecno HSL, Samsung Galaxy T5 prime 1, KZG min 1, wakati wakijua kuwa ni kosa kisheria.

Mwendesha mashtaka huyo amedai simu zote mali ya TCRA zina thamani ya Sh4,570,000.

Amesema baada ya Abdallah kuiba simu hizo alimpa Fatuma kwena kuziuza na kwamba moja kati ya simu hizo alimuuzia Bago.

Katika shtaka la pili, mwendesha mashtaka huyo amedai Agosti 27, 2018, saa tano usiku maeneo ya Ubungo, Bago alikutwa na simu aina ya Samsung Galax T5 prime yenye thamani ya Sh700,000 mali ya TCRA.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana akiwemo Bago.

Hakimu Marko Mochiwa, ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 8,2018  itakaposikilizwa tena huku washtakiwa hao wakiwa nje kwa dhamana.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz