Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshtakiwa adai aliwekewa dawa za kulevya kwenye begi na mumewe

DAWA ZA KULEVYA 2 Mshtakiwa adai aliwekewa dawa za kulevya kwenye begi na mumewe

Fri, 21 Oct 2022 Chanzo: mwanachidigital

Mshtakiwa, Sonia Kombo amedai kuwa mume wake, Mohamed Yusufu, ndio aliyeficha dawa aina ya heroine zenye uzito wa kilo 7.54 ndani ya mabegi yake mawili ya nguo ambayo walikuwa wanasafiri nayo kutoka Tanzania kwenda nchini India.

Hayo yamelezwa leo Okotba 20, 2022 na wakili wa Serikali, Caroline Materu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ritha Tarimo, wakati akiwasomea maelezo ya mashahidi na idadi ya vielelezo (Commital Proceedings) washtakiwa hao, kabla ya kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa.

Wanandoa hao ambao ni wakazi wa Zanzibar, wanadaiwa kutenda kosa hilo Agosti 11, 2021 Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Terminal 3 ambapo walikutwa na dawa hizo.

Akisoma maelezo ya onyo, mshitakiwa Sonia anadaiwa Septemba 11, 2021, akiwa JNIA sehemu ya kuondokea abiria, alipitisha mabegi yake mawili katika mashine ya kukagulia mizigo ndipo mkaguzi alitilia shaka baada ya kuona vitu visivyo vya kawaida kupitia mashine ya ukaguzi.

Wakili Materu amedai kuwa Sania akiwa kituo cha polisi alikiri kuwa alikuwa anasafiri na mabegi, lakini alikuwa hajui kama kuna dawa za kulevya ndani yake kwani mabegi hayo waliyabadilisha Dar es Salaam baada ya kufika kwa wenyeji wa mume wake.

Amedai wakati anatoka Zanzibar alikuwa na begi dogo lenye uwezo wa kubeba vitu vichache ambalo alikuwa anasafiri nalo kila mara, lakini alipofika Mbezi walikutana na mwenyeji wao Sheikh Rashid ambayo walilala kwake.

Amedai kuwa katika chumba cha mwenyeji wake alichopewa apumzike, ndani yake kulikuwa na mabegi mawili na vitu vingine na wakati wako eneo hilo walimueleza kwamba abadilishe begi lake ili vitu vyake vikae vizuri na ndipo mume wake alimbadilishia bila kufahamu kama kuna dawa za kulevya.

Ameeleza kwamba walipofika uwanja wa ndege, eneo la kukaguliwa, begi moja liliweza kupita lakini moja lilitiliwa shaka.

Baada ya hali hiyo, ofisa wa ukaguzi wa JNIA alimchua Sonia hadi alikokuwa mume wake kisha mabegi yalifunguliwa na kukutwa na dawa za kulevya.

Kwa upande wa maelezo ya onyo ya mshitakiwa Yusuph, Wakili Materu amedai kuwa yeye alikuwa anasafiri na mabegi hayo huku alikuwa anafahamu kuwa ndani yake kuna madawa ya kulevya lakini alimficha mke wake kwani aliyemuagiza mzigo huo alimweleza hivyo.

Amedai kuwa mashahidi ambao ni wahudumu wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere upande wa terminal 3 walidai kuwa walipata wasiwasi baada kuona mashine ukaguzi wa mizigo zikionyesha kuna kitu katika mabegi hayo.

Baada ya hapo wahudumu hao waliamua kumuita muhusika wa mabegi hayo na kumpeleka katika chumba cha ukaguzi pamoja na mabegi yake.

Wakaguzi walimuuliza mshitakiwa Yusuph kuwa nini kilichopo katika begi lake, naye aliwajibu kuwa kuna nguo na vitafunwa.

Inaelezwa kuwa baada ya kudai hayo, wakaguzi walitoa kila kitu kwenye mabegi hayo na kuyapitisha tena katika mashine na kukuta zile picha bado zinaonekana upande wa juu na wa chini ya mabegi hayo.

Amedai kuwa waaliamua kuyachana katika pande hizo na kukuta bahasha zikiwa zimefungwa vizuri kwa gundi nzito ndani zikiwa na chenga chenga ambazo zilidhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.

Ilidaiwa kuwa waliviweka vielelezo hivyo katika mifuko miwili vikiwa na vielelezo vingine na kuvifikisha kituo cha Polisi eneo hilo la Airport kwa ajili ya uchunguzi.

Wakili Materu amedai baada ya hapo Mkemia Mkuu wa Serikali alipima unga huo na kubainika kuwa ni kweli ulikuwa ni dawa za kulevya aina ya heroine yenye uzito wa kilo 7.54

“Mheshiwa hakimu upande wa mashtaka tunatarajia kuleta mashahidi 13 na vielelezo kadhaa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hawa,” amedai Wakili Materu.

Hakimu Tarimo baada ya kusikiliza kesi hiyo, amesema kwa Mamlaka aliyonayo anaihamishia kesi hiyo Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu uchumini na Makosa ya Rushwa kwa ajili ya kuanza kusikiliza wa ushahidi wa mashihidi wa upande wa mashtaka.

Baada ya maelezo hayo, washtakiwa hao wamerudishwa rumande wakisubiri kupangiwa tarehe na mahakama kwa ajili usikilizwaji.

Chanzo: mwanachidigital