Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshitakiwa kesi ya  ulaghai mil 717/- afariki

Ed41b4ab6bbd16d11ef986cc7bce48bd.jpeg Mshitakiwa kesi ya  ulaghai mil 717/- afariki

Thu, 20 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeelezwa kuwa, mshtakiwa katika kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Mkurugenzi wa Kampuni ya Balangai Estate Limited, Deryck Tweedey amefariki dunia.

Upande wa utetezi katika kesi hiyo uliieleza Mahakama hiyo jana mshitakiwa huyo alifariki dunia Mei 15, mwaka huu.

Wakili wa utetezi, Ndurumah Majembe alisema hayo jana wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi. Upande wa mashitaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Nguka Faraji.

"Mheshimiwa nimepokea taarifa ya kifo cha mteja wangu kilichotokea Mei 15, 2021 sasa hivi tuko kwenye taratibu za mazishi. Nawasilisha barua ya Mei 15, 2021 kutoka Hospitali ya Kairuki kama uthibitisho wa kutokea kwa kifo hicho wakati tunashughulika kupata cheti cha kifo," alieleza Majembe.

Awali, Wakili Faraji aliieleza kuwa, kesi hiyo ilipelekwa mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa ushahidi lakini shahidi wake alikuwa anaumwa na amepewa mapumziko ya siku tatu na kuomba wapangiwe tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo, Wakili Majembe alitoa taarifa juu ya kifo cha mshitakiwa huyo.

Wakili Faraji alitoa pole na kusisitiza upande wa utetezi uwasilishe cheti cha kifo ili kuthibitisha . Hoja hiyo iliungwa mkono na kusisitizwa na Hakimu Shaidi.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 21, mwaka huu.

Katika kesi hiyo, mshitakiwa alikuwa akidaiwa kuwa, Desemba 9, 2016 jijini Dar es Salaam, kwa ulaghai alimshawishi Gulam Dewji kumpatia Ebrahim Shamji Sh milioni 717.

Chanzo: www.habarileo.co.tz