Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshauri wa kodi kizimbani kwa kuisababishia TRA hasara

Hasara Kizimban TRA.png Mshauri wa kodi kizimbani kwa kuisababishia TRA hasara

Thu, 2 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

. Mshauri wa Kodi, Denis Tililo (29) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala akikabiliwa na mashtaka nane kikiwemo la kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya zaidi ya Sh118.9 milioni.

Tililo ambaye ni mkazi wa eneo la Msingwa jijini Dar es Salaam, amesomewa mashtaka yake na wakili wa Serikali, Theresia Mtao akisaidiana na Auni Chilamula pamoja na Emmanuel Medalakini ambao ni mawakili wa TRA mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rehema Lyana.

Katika kesi hiyo mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka nane kati ya hayo sita ya kutoa risiti za uongo kutoka kwenye mashine ya Kielektroniki (EFD), moja la kuisababishia TRA hasara na lingine la utakatishaji wa fedha zaidi ya Sh118.9 milioni.

Matao alidai kuwa kati Agosti 28, 2023 maeneo ya Buguruni wilayani Ilala mshtakiwa huyo alitoa risiti ya uongo kutoka kwenye mashine ya EFD iliyosajiliwa kwa jina la Yasini Revelian kwa nia ya kumdanganya Kamishna Mkuu wa TRA kwa ajili ya kumlipa mfanyabiashara hewa aitwae Janeth Kitego mwenye namba ya mlipakodi (TIN) namba 143-472-604 kodi ya Ongezeko la thamani ya Sh7.6 milioni

Katika shtaka lingine anadaiwa tarehe hiyo na maeneo hayo mshtakiwa huyo alotoa risiti ya uongo yenye namba 342 kutoka kwenye mashine ya EFD iliyosajiliwa kwa jina la Revelian kwa lengo la kumdanganya Kamishina Mkuu wa TRA kumlipa Kitego VAT ya Sh30.5 milioni.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa alitoa risiti ya uongo yenye namba 343 kutoka kwenye mashine EFD iliyosajiliwa kwa jina la Revelian na kumdanganya Kamishna Mkuu kumlipa Kitego VAT ya Sh27,457,627.12.

Mtao alidai mshtakiwa huyo alitoa risiti ya uongo yenye namba 343 kupitia mashine ya EFD ya Revelian kwa lengo la kumdanganya Kamishna Mkuu kuwa anamlipa mfanyabiashara hewa ambaye ni Kitego mwenye TIN namba 143-472-604 Kodi ya Ongezeko la thamani Sh27.4 milioni.

Katika mashtaka mengine inadaiwa mshtakiwa huyo alitoa risiti ya uongo namba 344 kwa kutumia mashine hiyo yenye kiasi cha Sh 780 milioni na kupotosha mfumo wa kodi wa TRA kwa lengo la kumdanganya kamishina ili kumlipa Kitego VAT ya Sh118,983,050.85.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo kwa makusudi aliisababishia TRA hasara ya zaidi ya Sh 118.9 milioni kwa kutoa risiti za uongo ambazo zilikuwa zinalenga kutoa taarifa za uongo kwa kamishina pamoja na mfumo wa mamlaka hiyo.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, mshtakiwa huyo anadaiwa kufanya miamala ya fedha ya Sh118,983,050.85 wakati akijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa la uhalifu wa kutumia risiti zisizo halali.

Upelelezi wa kikodi katika shauri hilo bado haujakamilika hivyo wameiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Lyana ameahirisha shauri hilo hadi Novemba 14, 2023 kwa ajili ya kutajwa na kumtaka mshitakiwa kurudi mahabusu kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kwamba moja ya shtaka linalomkabili ni la utakatishaji fedha halina dhamana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live