Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshauri akwamisha kesi ya wizi wa simu za TCRA

Tue, 25 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Kinondoni imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya wizi wa simu 17, mali ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) inayomkabili mlinzi wa mamlaka hiyo Rashid Abdallah na wenzake wawili kutokana na mmoja wa washauri wa mahakama kutokuwepo.

Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka kutokana na kukamilika kwa upelelezi lakini kutokana na kutokuwepo kwa mshauri huyo wa mahakama, leo Septemba 23,2018 mahakama hiyo imeshindwa kuendelea na badala yake imeahirisha hadi Oktoba 1, 2018.

Katika kesi hiyo Abdallah na wenzake, Fatuma Rajabu, mkazi wa Ubungo na Idd Bago, mkazi wa Ubungo Kibo, wote kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashtaka mawili, ikiwemo ya wizi wa simu 17 na kukutwa na simu ya wizi.

Washtakiwa hao walipopandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Septemba 17, 2018 na kusomewa mashtaka na washtakiwa wawili, Fatuma na Abdallah walikana mashtaka lakini Bago alikubali kosa.

Mwendesha mashtaka, Januari Kosekwa aliieleza  mahakama upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na akaomba mahakama ipange tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Hakimu Marko Mochiwa, aliwaachia kwa dhamana Abdallah na Fatuma baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wanne na kila mmoja kusaini bondi ya Sh5 milioni na akaamuru mshtakiwa aliyekiri kosa, Bago apelekwe mahabusu, huku akipanga kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Hata hivyo, baada ya kesi hiyo kuitwa, mwendesha mashtaka, Kusekwa, aliieleza mahakama kuwa ingawa kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa leo lakini mmoja wa washauri wa mahakama hayupo.

Hivyo aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine na Hakimu Mochiwa alipanga kesi hiyo ianze kusikilizwa Oktoba 1,2018.

Awali, akiwasomea mashtaka, mwendesha mashtaka, Kusekwa alidai Januari 9, 2018 saa 6 mchana katika ofisi za TCRA mlinzi Abdallah aliiba simu 17 aina ya KZG mobile phone 6 Dougeex51, Tecno HSL, Samsung Galaxy T5 prime 1, KZG min 1 huku wakijua ni kosa la kisheria.

Kusekwa amedai simu zote hizo ambazo ni mali ya TCRA zina thamani ya Sh4,570,000.

Alidai Abdallah baada ya kuiba simu hizo alimpa Fatuma aende akaziuze na  moja kati ya simu hizo alimuuzia Bago.

Katika shtaka la pili, Kusekwa alidai Agosti 27, 2018 saa 5 usiku maeneo ya Ubungo, Bago alipatikana na simu aina ya Samsung Galax T5 prime yenye thamani ya Sh700,000 ambayo iliibiwa na ni mali ya TCRA.

Chanzo: mwananchi.co.tz