Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshahara wa mke wa ‘mhasibu’ Takukuru wachambuliwa

24738 Pic+mhasibu TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shahidi wa tatu katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato  inayomkabili aliyekuwa mhasibu mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai na wenzake, ameieleza mahakama kuwa mke wa mshtakiwa huyo, Linda Ijumba alilipwa jumla ya Sh 167,581,797.

Amesema Linda ambaye pia alikuwa mtumishi wa Takukuru alilipwa fedha hizo kama  posho na mshahara tangu alipoajiriwa na taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa Julai 2002 hadi Desemba 2016, alipoacha kazi.

Kiasi hicho cha fedha  kinajumuisha posho na mshahara aliolipwa Linda kwa kipindi chote cha utumishi wake wa umma akiwa kama Katibu Muhtasi wa Takukuru.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Oktoba 30, 2018 katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na shahidi wa tatu katika kesi hiyo, Naza Alawi (43) kutoka Takukuru makao makuu mjini Dodoma.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Vitalis Peter mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Alawi amedai kuwa

kiasi hicho cha fedha ni mshahara, posho ya matibabu, posho ya mazingira magumu ya kazi, posho ya nyumba na posho ya uchunguzi tangu Linda alipoajiriwa na Takukuru.

Akifafanua kiasi hicho cha fedha alizolipwa Linda na mwajiri wake, Alawi  ambaye ni ofisa mchunguzi mwandamizi daraja la kwanza, amedai katika kipindi cha Julai 2002 hadi Desemba 2016, Linda alilipwa mshahara pekee kiasi cha Sh 41, 255, 488.

 

"Linda alianza na mshahara wa Sh68,000 Julai 2002 na baadae mshahara huo uliongezeka na kufikia Sh151, 851  lakini hadi anaacha kazi Takukuru,  Desemba 2016  alikuwa analipwa mshahara wa Sh555, 500 kwa mwezi,” amedai Alawi.

 

Amesema kuanzia Julai 2002 hadi Desemba 2016,  Linda alilipwa mshahara pekee kiasi cha Sh 41, 255, 488.

Amedai Linda alianza kulipwa posho ya matibabu ya Sh 100,000 kila mwezi kuanzia Julai 2006 hadi 2013, posho ya nyumba alilipwa Sh 25,000 kwa kila mwezi na posho ya mazingira  magumu ya kazi ilikuwa Sh 30,000 na baadae iliongezeka na kufika Sh 198, 550 hadi Julai 2011.

Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa jumla ya posho ya mazingira magumu ya kazi alizolipwa Linda kwa kipindi cha miaka 14 ya utumishi wake akiwa Takukuru ilikuwa ni Sh 27,407,849.

 

"Pia,  katika kipindi hicho cha miaka 14, Linda alilipwa na Takukuru posho ya matibabu kiasi cha Sh 8.4 milioni huku posho ya nyumba katika kipindi hicho ikiwa ni Sh 6, 968, 589."amedai Alawi.

Alibainisha mbali na fedha hizo, malipo mengine ya Linda ni nauli, pesa ya kusafiria mzigo wakati wa ajira yake ya kwanza,  likizo, gharama ya uhamisho marejesho ya matibabu,  safari za nje na mikopo yake ambapo alilipwa jumla ya Sh 40, 199, 910.

Nyingine ni posho ya uchunguzi kiasi cha Sh 43, 350,000, ambapo fedha hizo zililipwa kwa kusaini ofisini.

Shahidi huyo amedai kuwa baada ya Gugai kufukuzwa kazi, alipewa maelekezo na mhasibu mkuu wa Takukuru,  Ismail Othman kuchambua mishahara na posho alizolipwa  wakati anaajiriwa Gugai na Linda.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi  Novemba 12 na 14, 2018.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera.

Katika kesi ya msingi, Gugai na mwenzake, wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali ambalo linamkabili Gugai.

Gugai anakabiliwa na kosa la kumiliki mali kinyume na kipato chake, ambapo alitenda kosa hilo kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

Inadaiwa kuwa akiwa Takukuru Dar es Salaam, Gugai alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni ambazo hazilingani na kipato chake huku akishindwa kuzitolea maelezo.

Chanzo: mwananchi.co.tz