Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshahara wa ‘mhasibu’ Takukuru wachambuliwa

24657 Mshahara+pic TanzaniaWeb

Wed, 31 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shahidi wa tatu katika kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato, inayomkabili aliyekuwa mhasibu mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai na mwenzake, ameieleza Mahakama kuwa jumla ya fedha halali alizolipwa mshtakiwa huyo tangu aajiriwe ni Sh334,175,332.

Shahidi huyo, Naza Alawi (43)kutoka Takukuru Makao Makuu, Mkoa wa Dodoma ameeleza hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati akitoa ushahidi dhidi ya Gugai aliyeajiriwa Julai 2001 na ajira yake kuisha Agosti 2016.

Alidai kuwa kipato hicho cha fedha alicholipwa na mwajiri wake, hakiendani na mali anazomiliki ambazo ni zaidi ya Sh3.6 bilioni.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Vitalis Peter akisaidiana na Pius Hila, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, shahidi huyo alidai kuwa kiwango hicho ni mshahara, posho ya matibabu, mazingira magumu ya kazi na nyumba.

Akifafanua fedha alizolipwa Gugai na mwajiri wake, Alawi ambaye ni ofisa mchunguzi mwandamizi daraja la kwanza, alidai kuwa kuanzia Julai 2001 hadi Agosti 2016, Gugai alilipwa mshahara pekee Sh218,916, 859.

Pia, katika kipindi hicho hicho, Gugai alilipwa Sh99,944,000 ambazo ni posho ya mazingira magumu ya kazi.

“Agosti 2006 hadi Juni 2013, Gugai alilipwa na Takukuru posho ya matibabu Sh12,450,000, huku posho ya nyumba katika kipindi hicho ikiwa ni Sh2, 864, 372,” alidai Alawi.

Shahidi huyo ambaye pia anasimamia dawati la mshahara tangu Februari 2005, alidai kuwa kosa lililosababisha Gugai kufukuzwa kazi ni kukutwa na mali nyingi ambazo hakuzitolea tamko katika fomu ya mali.

Alida kuwa Gugai alianza kulipwa mshahara wa Sh152,630 Julai 2001 na baadaye mshahara wake uliongezeka na kufikia kiasi cha Sh 191,822, Februari 2004.

“Mpaka anafukuzwa kazi Agosti 2016, alikuwa anapokea mshahara wa Sh4,417,838,” alidai Alawi ambaye ana shahada ya uzamili ya biashara na utawala.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasin Katera ambao wanakabiliwa na makosa 43, kati ya hayo 19 ni ya kughushi, 23 ni utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali, ambalo linamkabili Gugai.

Chanzo: mwananchi.co.tz