Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msako zaidi mtuhumiwa wa Takukuru

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imeagiza mtuhumiwa wa utakatishaji fedha, Magreth Kobelo Gonzaga anayedaiwa kutorokea nje ya nchi ajisalimishe haraka iwezekanavyo kabla haijachukua hatua za kumrudisha nchini kwa nguvu.

Hayo yameelezwa ikiwa ni siku moja tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kumtaka ajisalimishe haraka ili kujibu tuhuma za kujihusisha na utakatishaji wa fedha haramu kabla mali zake hazijataifishwa.

Akizungumza na wanahabari jana, Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi alisema kuna sheria za kimataifa na za nchi kushirikiana kuwarejesha watu ambao wanakabiliwa na mashtaka katika nchi moja na wakakimbilia nchi nyingine.

“Wanaweza kuwa ni raia wa nchi nyingine au hata raia wa Tanzania. Kwa mfano, hapa Tanzania tumekwishapokea maombi kutoka nchi zingine kuwarejesha wahalifu kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa niseme wazi hayuko salama kwa sababu jumuiya yote inashirikiana kupambana na uhalifu,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema kutokana kuimarika kwa miundombinu ya usafiri kama wa ndege na mawasiliano, kuna makosa ambayo yanaweza kufanyika nchi moja lakini yakaidhuru nchi nyingine kwa hiyo nchi zote zinashirikiana.

Alisema atakapobainika alipo, maombi rasmi yatatumwa na ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Mambo ya Nje ili arudishwe na afikishwe katika mahakama.

“Watanzania tunaona kukwepa kodi ni jambo dogo sana, hakuna makosa makubwa ambayo Marekani na Ulaya yanaogopwa kama kodi, kosa la kodi ni kubwa katika nchi hizo... ni kosa kubwa mno lazima arejeshwe, na haki itendeke,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz