Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msako wa polisi waua watuhumiwa watatu wa ujambazi Kigoma

46308 PIC+POLISI Msako wa polisi waua watuhumiwa watatu wa ujambazi Kigoma

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kibondo. Watu watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi wameuawa huku wengine wakifanikiwa kukimbia baada ya kuibuka kwa majibizano ya risasi na polisi katika msako wa kuwatafuta watekaji wa magari katika pori ya Moyowozi mkoani Kigoma.

Jeshi la  polisi liliingia katika msako wa kuwasaka wahalifu hao baada ya kupata taarifa za vitendo vya utekaji wa gari aina ya Land Cruiser mali ya Shirika la Good Neighbour linalohudumia wakimbizi, lililokuwa linaendeshwa na Machumu Ikombe (34), akiwa na mfanyakazi wa shirika hilo raia wa Korea, Soiji Oh (26).

Akizungumza leo Jumatatu Machi 12, 2019 kamanda wa polisi mkoani Kigoma, Martin Ottieno, amesema tukio hilo limetokea juzi Jumapili Machi 10, 2019 saa 2:15 asubuhi katika kijiji cha Nyarulanga wilayani Kibondo mkoani Kigoma.

Amesema baada ya jeshi hilo kupata taarifa hizo iliingia katika pori hilo na kuanza kufanya msako saa 12 jioni walifanikiwa kuwaona na kuwataka wajisalimishe lakini walikaidi na kuanza kuwashambulia askari kwa risasi.

Amesema baada ya kuona wahalifu hao wameanza kuwashambulia ndipo askari nao wakajibu mashambulizi hayo na kuwajeruhi watu watatu na kufariki dunia wakiwa njiani kupelekwa hospitali ya wilaya ya Kibondo huku wengine wakifanikiwa kukimbia.

"Katika pori hilo pamoja na kuwakamata wahalifu hao tumekamata begi lenye vitu mbalimbali ikiwemo kompyuta mpakato 1 aina ya HP, simu za mkononi 10, chaji 1, tochi 2, chaji za kobe 2, betri 1, viatu pea 2, shuka la kimasai 1, tisheti 1 na fedha Sh2,300," amesema kamanda Ottieno.

Aidha kamanda Ottieno amewataka wananchi waliopoteza mali zao kwa matukio ya wizi kutoa taarifa katika kituo cha polisi kwa ajili ya kutambua mali zao.

Katika tukio hilo watu hao waliokuwa wakidhaniwa ni majambazi waliteka gari hilo na kupora vitu mbalimbali pamoja na kompyuta mpakato 1 yenye thamani ya Sh2.5 milioni, simu ya mkononi, fedha taslimu Sh230, 000 na begi moja likiwa na vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh454, 000. Jumla ya vitu vyote ni zaidi ya Sh3.3 milioni.



Chanzo: mwananchi.co.tz