Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msako wa noti bandia wa DC Sabaya ulivyomuibua Dar

89071 Sabayapic Msako wa noti bandia wa DC Sabaya ulivyomuibua Dar

Thu, 19 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Noti bandia za thamani ya zaidi ya Sh500 milioni kama zingekuwa halisi,  na mitambo ya kuzitengenezea zimekamatwa jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo limefanywa jana Jumanne Desemba 17, 2019 na Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga ambaye alipendekeza adhabu kali kwa wanaohusika na vitendo hivyo.

Mkazi wa  Chanika, Masumbuko Paulo na wenzake wawili walikamatwa baada ya kufanyika uchunguzi kwa kushirikisha wadau mbalimbali ikiwa ni siku chache tangu mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kuendesha operesheni ya kusaka fedha bandia na kumkamata Richard Mtui na Sh13 milioni.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa na kiasi hicho cha fedha Oktoba 19, 2019 katika mji wa Bomang'ombe akijiandaa kuzisambaza mtaani.

Jana wakati akitoa taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao  wanaojihusisha na utengenezaji wa fedha bandia, Profesa Luoga alimpongeza Sabaya aliyekuwepo katika mkutano huo, na kueleza namna fedha hizo bandia zinavyoweza kuathiri uchumi.

"Kipekee ninamshukuru Sabaya ambaye wiki chache zilizopita alikamata fedha bandia. Juhudi hizo zilituwezesha sisi wenye  jukumu la kulinda uchumi wa nchi kujua tatizo ambalo nchi ilikuwa inakabiliana nalo,  halikuwa la kawaida,” amesema Profesa Luoga.

Profesa Luoga amesema bila kulinda uchumi, nchi inaweza  kuhujumiwa.

Kuhusu adhabu, Profesa Luoga amesema kwa sasa adhabu ya kifungo inayotolewa ni ndogo ikilinganishwa na kosa lenyewe, akibainisha kuwa ipo haja ya kuanzisha majadiliano kuhakikisha adhabu dhidi ya wanaopatikana na makosa ya kutengeneza fedha haramu inakuwa kubwa.

“Kuna haja ya kuanza majadiliano kuhakikisha adhabu ya upatikanaji na utengenezaji wa fedha haramu inakuwa kubwa,” amesema.

“Suala la adhabu ni la mahakama, lakini kwa uhalifu wa namna hii ni mbaya na unahitaji adhabu ya kutosha itakayoendana na kosa lenyewe kwa kuwa zipo nchi zinazotoa adhabu ya kunyonga kwa makosa ya uhujumu uchumi,” amesema.

Profesa Luoga alibainisha kuwa tatizo ambalo nchi ilikuwa inakabiliana nalo si la kawaida. BoT ilichukua hatua kwa kulinda noti bandia zisiingie kwenye benki.

Amesema  vyombo vya dola viliingia na kuhakikisha wanatambua mahali fedha haramu imetumika.

“Bila kuhakikisha uchumi unalindwa nchi inaweza kuhujumiwa. Moja ya hujuma ni fedha za kigeni kushambuliwa na hii hufanyika pale Benki Kuu inaposhindwa kuweka udhibiti,” alisema.

Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha imekuwa na matukio mengi ya kukamatwa kwa fedha bandia, jambo linalotajwa kuwa na athari katika uchumi wa nchi.

Chanzo: mwananchi.co.tz