Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mrembo mbaroni kwa tuhuma mauaji ya mwanaume aliyelala naye

Mauaji Nn.jpeg Mrembo mbaroni kwa tuhuma mauaji ya mwanaume aliyelala naye

Tue, 20 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkazi wa Kijiji cha Kiroka, wilayani Morogoro, Salipina Thomas (21), anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji baada ya mwanaume aliyekuwa amelala nyumbani kwake, Rashid Maharagande, kuuawa na mtu aliyetoweka.

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, SACP Fortunatus Musilimu, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema lilitokea Septemba 17, mwaka huu, majira ya saa nane usiku kitongoji cha Temekero, Kijiji cha Kiroka, Tarafa ya Mkuyuni.

"Kijana Richard Stephen Chanzila (23), mkazi wa kitongoji cha Maembe, Kijiji cha Kiroka, ndiye anatuhumiwa kufanya mauaji hayo kwa kumkata kwa kitu chenye ncha kali shingoni kijana Maharagande, mkazi wa Sultan Area, Manispaa ya Morogoro aliyekuwa pia akijishughulisha na kazi ya bodaboda," alisema Musilimu.

Alisema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi baada ya Maharagane kukutwa amelala ndani ya nyumba ya Salipina, aliyekuwa na mahusiano naye ya kimapenzi.

Kamanda alisema baada ya mtuhumiwa kuwakuta wamelala, aliamua kumkatakata kwa kitu chenye ncha kali Maharagande sehemu ya shingoni.

Alisema wakati mwanamke huyo akikimbia kutafuta msaada, mtuhumiwa Chanzila aliubeba mwili wa marehemu na kuondoka nao kwenda kuutupa porini umbali wa karibu mita 100 kutoka eneo yalikofanyika mauaji.

Kamanda alisema mtuhumiwa anayedaiwa kuwa ni mzazi mwenzie Salipina, alitoroka kijijini hapo kwenda kusikojulikana baada ya mauaji hayo na polisi wanaendelea na msako ili kumtia mbaroni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Aliwasihi wananchi kuacha kushiriki mauaji ya aina mbalimbali ikiwamo yanayosababishwa na wivu wa kimapenzi, ushirikina au migogoro mingine kwa kuwataka wafuate njia sahihi za kupata suluhisho la migogoro yao.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Temekelo ‘A’ Banzi Bonzo, akizungumzia mauaji hayo, alisema: "Yule binti ni jirani yangu na anaishi kwenye mtaa wangu, binti alikuwa na mwanaume aliyekuwa amezaa naye, lakini waliishi kwa malumbano mara nyingi na mara ya mwisho tuliwapeleka kituo cha Polisi Mkuyuni baada ya mwanaume kumtishia mwanamke kisu.”

“Sijui kesi iliishaje, hadi usiku saa nane mzazi mwenzie naye alikuwa bado anamuwinda huyu binti bila kujua akamfuatilia na kuona ameingia na mwanaume mwingine kutoka Sultan Area mjini, ilikuwa hata hawajafanya kitu, akawavamia na kuwalazimisha kuvua nguo na kuanza kuwapiga mapanga, mwanamke akakimbia," alisema Banzi Bonzo.

Alidai majira ya saa moja asubuhi alifika jirani anayekaa karibu na nyumbani kwake na kutoa taarifa ya kuona damu nyingi nje ya nyumba yake.

Alisema, walipoifuatilia ilifika hadi mlangoni kwa binti, na walipomtafuta hakuwapo nyumbani kwake na kuamua kwenda kwa mama yake mzazi anayeishi jirani na kumkuta binti aliyedai kuwa alikuwa anataka kwenda kwake kumjuza yaliyojitokeza usiku.

"Nilimuuliza mbona hakuja kwangu, kama aliweza kwenda kwa mama yake? Kwa kuwa ni lazima kwanza apite kwangu, lakini alianza kwa mama yake ndiyo atake kuja kwangu?” Akasema alichanganyikiwa baada ya kuona mwenzake waliyelala naye anapigwa mapanga.”

“Nikaripoti Polisi tukio hilo wakaja kumchukua binti na baadaye kidogo watu walikuja kunieleza wameuona mwili umelala porini kwenye njia mpya, ikabidi tuwaarifu tena Polisi, wakaja kuchukua mwili," alisema Mwenyekiti huyo.

Mama mzazi wa binti huyo, Vaileth Hamis, alikiri kijana anayetuhumiwa kwa mauaji alikuwa akiishi na mwanawe na walipeana ujauzito, lakini hakuwahi kumuoa wala kumlipia mahari na hata hakuwahi kuhudumia mimba wala mtoto, jukumu ambalo alilifanya yeye kama mama wa binti.

"Wakati wa ujauzito wa binti yangu, yeye alikuwa jela alikopelekwa na baba yake mzazi baada ya kumfanyia maovu, akampeleka huko akajifunze," alisema Vaileth.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live