Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Mr Kuku’ kortini bil 17 za upatu

5c6775b860a2a9a0b76922f1a9cffd50 ‘Mr Kuku’ kortini bil 17 za upatu

Tue, 11 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MFANYABIASHARA Tariq Machibya (29) maarufu Mr Kuku, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka saba likiwemo kufanya biashara ya upatu na kutakatisha fedha wa Sh bilioni 17.

Kijana huyo mkazi wa Oysterbay jijini humo alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mfawidhi, Godfrey Isaya.

Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai katika mashitaka ya kwanza kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2018 na Mei mwaka huu maeneo ya jiji la Dar es Salaam, mshitakiwa alifanya na kusimamia biashara ya upatu kwa kukusanya fedha toka kwa umma.

Imedaiwa mahakamani kuwa Machibya alifanya biashara hiyo kwa ahadi kwamba zimewekwa kwenye biashara ya kuku na watu wangepata asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 kwa mtaji wa awali uliowekezwa kwa miezi sita kiasi ambacho ni kikubwa kuliko mtaji uliokusanywa.

Simon alidai kuwa, kati ya Januari 2018 na Mei mwaka huu maeneo ya jiji la Dar es Salaam, Machibya alipokea fedha kutoka kwa umma ambazo ni Sh bilioni 17 bila kuwa na leseni.

Ilidaiwa kuwa kati ya Aprili 26, 2019 na Januari 26 mwaka huu maeneo ya jiji hilo, mshitakiwa alijihusisha na miamala ya Sh 6,477,297, 614.83 kwa kutoa kutoka kwenye akaunti ya CRDB ya Mr Kuku Farmers Ltd huku akifahamu kuwa fedha hizo ni zao la kosa la kusimamia biashara ya upatu.

Pia ilidaiwa mahakamani kuwa, kati ya Januari 17 mwaka huu na Machi 30 mwaka huu katika maeneo hayo, Machibya alijihusisha na miamala ya Sh 629, 249, 576.36 kwa kutoa fedha hizo katika akaunti ya CRDB wakati akifahamu fedha hizo ni zao la biashara ya upatu.

Kati ya Machi 5 mwaka huu na Aprili 17 mwaka huu maeneo ya Dar es Salaam, mshitakiwa alijihusisha na miamala ya Tsh 1,366,718,048.46.

Katika shitaka la sita, Simon alidai kati ya Januari 17 mwaka huu na Januari 30 mwaka huu maeneo ya CRDB Viva Tower iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam Machibya alijihusisha na miamala ya Dola za Marekani 107,893.73 na kuingiza fedha hizo kwenye akaunti ya CRDB.

Ilidaiwa kuwa kati ya Machi 3 na 30 mwaka huu maeneo ya CRDB Waterfront mshitakiwa alijihusisha na kuingiza Dola za Marekani 146,300 kwenye akaunti ya Mr Kuku Farmers Ltd.

Mshitakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. Upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Isaya aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 24, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshitakiwa amerudishwa rumande kwa sababu mashitaka yanayomkabili hayana dhamana.

Chanzo: habarileo.co.tz