Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpemba wa Magufuli, wenzake bado wanajadiliana na DPP

86347 Mpembapic Mpemba wa Magufuli, wenzake bado wanajadiliana na DPP

Fri, 29 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Yusuf Ali Yusuf  maarufu Mpemba wa Magufuli na wenzake imekwama kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi Novemba 28, 2019.

Kesi hiyo ilipangwa kuendelea na ushahidi lakini upande wa mashtaka umeieleza mahakama hiyo kuwa hawana shahidi kwa sababu washtakiwa wapo katika majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Yusuf na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manne ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo ya Sh785.6 milioni.

Wakili wa Serikali, Salim Msemo ameeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba  wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

"Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa, upande wa mashtaka hatuna shahidi kwa sababu washtakiwa wapo katika mazungumzo  na DPP," amedai Msemo.

Washtakiwa hao walimuandikia DPP barua ya kukiri na kuomba msamaha Oktoba, 2019.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka  aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 11, 2019.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Yusuph, washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni Charles Mrutu, Benedict Kungwa, Jumanne Chima, Ahmed Nyagongo na Pius Kulagwa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na mtandao wa ujangili, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 53/2016.

Miongoni mwa shtaka moja kati ya manne yanayowakabili washtakiwa hao ni kujihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya dola 180,000 sawa na Sh392,817,600 bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.

Chanzo: mwananchi.co.tz