Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mpakistan aliyefungwa kesi ya dhahabu kufukuzwa nchini

49290 PAKIST+PIC

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

 Mwanza. Mmoja wa washtakiwa wanne waliohukumiwa kifungo jela cha kati ya miaka mitano hadi 15 pamoja na faini ya Sh5 milioni hadi Sh100 milioni atafukuzwa nchini mara baada ya kulipa faini au kumaliza kifungo.

Mshtakiwa huyo ambaye hata hivyo hakutajwa jina ni kati ya waliokiri kosa na kuhukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza iliyopewa mamlaka ya kusikiliza na kuamua kesi ya uhujumu uchumi namba 1/2019 dhidi ya washtakiwa 12, wakiwemo waliokuwa askari polisi wanane.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana,  Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga alisema mshtakiwa huyo ambaye kwa sasa ni mfungwa katika Gereza Kuu la Butimba jijini Mwanza ni raia wa kigeni ambaye licha ya kuingia nchini kihalali, ametiwa hatiani kwa kosa la jinai.

Waliohukumiwa adhabu hiyo ni wafanyabiashara Hassan Sadiq, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda na Sajid Hassan.

“Mmoja wa waliohukumiwa kifungo juzi ambaye ni raia wa kigeni ataondoka nchini mara moja baada ya kulipa faini au kumaliza kutumikia kifungo hata kama aliingia nchini kihalali, hawezi kuishi nchini akishiriki matukio ya kijinai,” alisema DPP.

Ingawa hakumtaja jina, lakini mshtakiwa Sajid Hassan ndiye raia wa kigeni miongoni mwa washtakiwa wanne waliokiri kosa na kuhukumiwa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Rhodha Ngimilanga.

Katika maelezo ya jumla ya makosa yaliyosomwa na Wakili wa Serikali Jacklyn Nyantori, mshakiwa huyo alielezwa kuwa ni raia wa Pakistan na alikutwa nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza Hassan Sadiq.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz