Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mosha aamriwa kuilipa NICOL mamilioni

Court Mosha aamriwa kuilipa NICOL mamilioni

Mon, 18 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwamuru aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Nicol, Felix Mosha pamoja na mshitakiwa mwenzake, Kathleen Armstrong kurejesha gari aina ya Toyota Land Cruiser na pia kuilipa Kampuni ya NICOL Sh 14,400,000 ambazo ni gharama zilizotumika kukodisha gari mbadala.

Pia amemariwa kulipa Sh milioni 22 kampyuni hiyo kiwango cha pesa ambacho yeye na mdaiwa mwenzake waliuza gari la kampuni bila kibali.

Kesi hiyo ya madai namba 282/2017 ilikuwa mbele ya Hakimu Yosto Ruboroga aliyetoa hukumu hiyo Oktoba 13 mwaka huu.

Kesi hiyo ilifunguliwa na wanahisa wa Kampuni ya Nicol dhidi ya Felix Mosha, Mwenyekiti wa Nicol aliyeondolewa madarakani pamoja na Kathleen Armstrong aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu ambaye kwa sasa anaishi Marekani.

Katika shauri hilo, hakimu alisema mahakama ilithibitisha kwamba kwa mujibu wa vilelezo pamoja na ushahidi uliotolewa, wadaiwa waliondolewa kihalali na wanahisa kwenye nafasi zao wakati wa mkutano mkuu wa wanahisa kutokana na ubadhirifu wa mali za kampuni.

Mahakama ilitoa uamuzi huo baada ya kuthibitisha kuwa sababu zilizotolewa na wadaiwa kwamba walirudishwa madarakani katika maamuzi yaliyotolewa na Jaji Fauz Twaibu, katika kesi No 16 ya 2011 si ya kweli na yenye kupotosha.

Alisema uamuzi wa Jaji Twaibu ulisema wazi kwamba amri yake isingeweza kuwa ya kudumu na hasa mara baada ya wanahisa kufikia uamuzi wa kuwaondoa madarakani wadaiwa na kuteua viongozi wapya, amri ile ilikufa.

Hivyo Hakimu alisema mahakama imeamua kwamba uamuzi wa wanahisa wa kuchagua viongozi wengine ulikuwa ni halali na ndio maana maamuzi hayo yalikubaliwa kama ilivyothibitishwa na maamuzi mbalimbali ya mahakama kuu, pia kwamba maamuzi hayo ya wanahisa ya Aprili 14, 2012, hayajawahi kubadilishwa na mahakama yoyote mpaka sasa.

Alisema mahakama imeamua Mosha na Armstrong warejeshe gari ya kampuni namba T. 133 AVG, Toyota Land Cruiser na pia kuilipa Nicol Sh 14,400,000 kama gharama zilizotumika kukodisha gari mbadala, kulipa Sh milioni 22 ambacho ni kiwango cha pesa alichouza gari ya kampuni bila kibali na pesa hizo kutokuonekana kwenye vitabu vya fedha vya kampuni, gharama za usumbufu Sh milioni 10 pamoja na gharama za kesi.

Katika shauri hilo, Kampuni ya Nicol iliwakilishwa na wakili Benjamin Mwakagamba wa ofisi ya uwakili ya BM wakati Mosha aliwakilishwa na wakili Dominic Daniel.

Chanzo: www.habarileo.co.tz