Arusha. Mmiliki wa shule ya msingi Lucky Vicent, Innocent Moshi amesema hana hatia katika kesi inayomkabili kutokana na ajali iliyosababisha wanafunzi wake 32, walimu wawili na dereva kufariki katika ajali iliyotokea mwaka juzi.
Akitoa ushahidi wake, jana Jumanne Machi 19, 2019 Mbele ya Hakimu mkazi, Niku Mwakatobe, alisema alipata taarifa ya kutokea ajali hiyo, Mei 6 mwaka 2017 kupitia mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Efrahim Jackson kuwa gari lililobeba wanafunzi limepata ajali.
Akiongozwa na wakili wake, Method Kimomogoro, Moshi alieleza mahakama baada ya taarifa hiyo walikutana na walimu mkuu na kuanza safari ya kuelekea sehemu ya ajali na walipofika katika sehemu ya ajali walikuta watu wengi wamezunguka katika ajali hiyo huku majeruhi na marehemu wakiwa wamepelekwa katika hospitali ya wilaya ya karatu.
Alisema walielekea kwenye hospitali ya Karatu na walipofika mwalimu mkuu alijitambulisha kwa askari na kuelekezwa sehemu ambayo marehemu wamehifadhiwa na walipofika katika chumba hicho maaskari walitaka kumjua dereva na tuliwaonesha dereva akiwa tayari amefariki .
Moshi alisema dereva alifahamika kwa jina la Dismas Kesy na hapo mkuu wa wilaya ya Karatu Theresia Mahonga alikuja kwa ajili ya kuwaona majeruhi na wakiwa katika hospitali ya karatu.
Hata hivyo, alisema Mi 9, mwaka 2017, alikamatwa na polisi na kuwekwa ndani kwa sababu ya ajali na baada ya siku tatu alipelekwa mahakamani na moja ya makosa alishitakiwa kwa kosa la kuendesha gari la wanafunzi kuwapeleka shuleni na kuwarudisha bila kuwa na leseni ya biashara.
Alisema pia alishitakiwa kwa kosa la kutumia gari bila kuwa na bima na kuwapakia wanafunzi 38 ndani ya basi dogo kinyume na sheria kwani linapasa kubeba abiria 25
Alisema yeye hajatenda makosa hayo pia kampuni ya lucky vicent iliuziwa gari yenye namba T871 BYX na Swalehe kiluva pamoja na kuwakabidhi kadi ya gari bima ya gari pamoja na leseni ya gari hilo.
Mshitakiwa wapili Mwalimu Mkuu msaidizi katika shule hiyo, Longino Vicent(40) alieleza mahakama kuwa Mei 6 waka 2017, alifika shuleni muda wa saa kumi na mbili asubuhi na kushughulikia zoezi la usafiri wa wanafunzi aliopewa na mwalimu mkuu na gari tatu kwenda Karatu.
Vicenti alikanusha kuhusika na ajali hiyo kwani hakuwepo eneo la tukio na yeye alitimiza wajibu wake aliokabidhiwa na mkuu wa shule kuwasafirisha wanafunzi hao wakiwa na walimu wao.
Kwa upande wa Wakili wa serikali Lilian Mmasi aliwauliza maswali washitakiwa hao juu ya maelezo yao ikiwepo kuwa wao ndio viongozi wa shule hiyo na walikubali.
Alimtaka mmiliki wa shule hiyo, Moshi kueleza kama kuna wakurugenzi wengine wa shule hiyo na kueleza kuwa wapi wanne .
Wakili wa utetezi Chimomogoro aliomba kufunga utetezi katika kesi hiyo na kuomba siku ya kuleta taarifa za mwisho za majumuisho ya kesi hiyo.
Hakimu Mwakatobe alipanga Aprili 3 mwaka huu ambapo Aprili 4 mwaka huu atapanga tarehe ya kusoma hukumu katika kesi hiyo.