Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mmiliki ukumbi wa Mrina, wenzake kortini tuhuma za uhujumu uchumi

89848 Ukmbi+pic Mmiliki ukumbi wa Mrina, wenzake kortini tuhuma za uhujumu uchumi

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfanyabiashara nchini Tanzania, Maiko Mrina (67) na wenzake wawili wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la  kuisababishia Serikali ya Tanzania hasara ya Sh30 milioni na kuiba nondo tani nane.

Mbali na Mrina, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi namba 140/2019 ni dereva, Ally Athumani (36) mkazi wa Mbagala na mlinzi Shabani Rashidi (57) mkazi wa Mwananyamala wote wa jijini Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo, Mrina amesomewa mashitaka yake hospitalini leo Jumanne Desemba 24, 2019 akiwa amelazwa wodi namba mbili katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) baada ya kuugua.

Washitakiwa hao walisomewa mashtaka na jopo la mawakili watatu wa upande wa mashtaka, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Vicky Mwaikambo.

Wakili wa Serikali Mkuu Mkunde  Mshanga akisaidiana na wakili wa Serikali mwandamizi Wankyo Simon na Grory Mwenda, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati Agosti 29 na 30, 2018 katika eneo la Ubungo.

Katika shtaka la kwanza, linalomkabili  Athumani pekee, anadaiwa akiwa mwajiliwa wa Kampuni ya China Civil Engineering Contraction Corporation aliiba tani nane za Nondo zenye thamani ya Sh30.40 milioni mali ya kampuni hiyo, zilizofika kwake kutokana na nafasi yake ya ajira.

Shitaka la pili ilidaiwa kati ya Agosti 29 hadi 30,2018 katika Jiji la Dar es Salaam, washitakiwa wote kwa nia ovu waliisababishia Serikali hasara ya Sh30.40 milioni

Katika shitaka la tatu inadaiwa, Agosti 29, 2018, washitakiwa kwa pamoja walitakatisha kiasi hicho cha fedha wakati wakijua fedha hizo ni mali ya kosa la wizi.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Mwaikambo  alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kutokana na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka kwa DPP.

Upande wa mashitaka ulidai, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na Hakimu Mwaikambo ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 7, 2020, itakapotajwa.

Washtakiwa wawili wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria, huku Mrina akiendelea kusalia hospitali hapo.

Chanzo: mwananchi.co.tz