Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mme wa Shamimu ajisalimisha kwa DPP

83809 Pic+shamimu Mme wa Shamimu ajisalimisha kwa DPP

Thu, 14 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mfanyabiashara, Abdul Nsembo maarufu Abdulkandida (45) ameandika barua ya kukiri kosa lake na kuomba msamaha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania(DPP).

Nsembo na mkewe, Shamimu Mwasha (41) wakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin, kinyume cha sheria, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Tanzania.

Soma zaidi:  Kesi ya Shamim, mmewe mambo ni yaleyale

Nsembo kupitia wakili wake, Benedict Ishabakaki, ameieleza mahakama hiyo leo Jumatatu Novemba 11, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Ishabakaki ameeleza hayo, muda mfupi, baada ya upande wa mashtaka kudai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

"Mteja wangu, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hii (Abdul Nsembo) amemuandikia DPP barua ya kuomba msamaha na kukiri shtaka lake, hivyo tunasubiri majibu," amedai Ishabakaki.

Akijibu hoja hiyo, wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai maombi ya mshtakiwa yanafanyiwa kazi na DPP, hivyo baada ya kufanyiwa kazi atapewa taarifa.

Kuhusu upelelezi kutokukamilika, wakili Simon alidai kuwa bado nasubiri ripoti ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Soma zaidi:  Kesi ya Shamimu na mumewe, bado Mahakama inasubiri ripoti ya Mkemia Mkuu

"Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka tunasubiri majibu ya kielelezo kilichopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," alidai Simon.

Baada ya kueleza hayo, hakimu Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 22, 2019 itakapotajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 36/2019.

Soma zaidi:  Kesi ya Shamimu na mumewe, Mahakama inasubiri ripoti ya Mkemia Mkuu

Kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha  dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gram 232.70, wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo, Mei mosi, 2019 katika eneo la Mbezi Beach, Jijini Dar Es Salaam.

Chanzo: mwananchi.co.tz