Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mlinzi aliyehukumiwa kuua Mwananfunzi akwepa kitanzi

Mlinziiiiiiiiiiiiiii Mlinzi aliyehukumiwa kuua Mwananfunzi akwepa kitanzi

Mon, 4 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama imemuachia huru aliyekuwa mlinzi wa Shule ya Sekondari Scolastica, iliyopo mji mdogo wa Himo wilayani Moshi, Hamis Chacha (34) aliyehukumiwa kifo kwa kosa la kumuua kwa makusudi mwanafunzi wa shule hiyo, Humphrey Makundi.

Chacha ameachiwa huru baada ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani Tanzania kusikiliza rufaa, kushusha shitaka lake kutoka mauaji ya kukusudia na kuwa ya bila kukusudia, baada ya kubaini hakuwa na nia ovu ya kuua.

Maelezo ya kosa hilo yanaeleza kuwa Septemba 6, 2017 saa 2 usiku, katika mji wa Himo, mlinzi huyo alimuua mwanafunzi Humphrey aliyekuwa kidato cha pili kwa kumpiga na ubapa wa panga.

Baada ya kesi kusikilizwa, Juni 3, 2019 Jaji Firmin Matogolo alimtia hatiani.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, siku hiyo (Septemba 6, 2017) mlinzi akiwa doria nje ya uzio wa shule, alisikia kishindo cha mtu kuruka ukuta kutoka ndani ya shule.

Alipofuatilia aliona mtu akikimbia, alimkimbiza na alipomkaribia alimpiga kwa ubapa wa panga lakini hakusimama.

Mlinzi aliendelea kumkimbiza, umbali mfupi baadaye, mtu huyo alianguka. Alimsogelea na kumpiga tena kwa ubapa wa panga, mtu huyo ambaye wakati huo hakuwa amemtambua hakuamka tena.

Mlinzi huyo alimpigia simu mmiliki wa shule, Edward Shayo na mwalimu wa nidhamu, Laban Nabiswa; walibaini mtu yule ni mwanafunzi Humphrey Makundi (16) na alikuwa amekufa, ndipo walijadiliana na kuamua kuutupa mwili katika Mto Ghona ulio jirani na shule. Mwili uligundulika Septemba 12, 2017 katika mto huo ukiwa umeanza kuharibika na ilibainika ni wa mwanafunzi huyo.

Shayo, Nabiswa na Chacha walikamatwa na kuhusishwa na mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi huyo.

Baada ya Mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, iliwaondoa Shayo na Nabiswa katika kosa la mauaji ya kukusudia na kuwatia hatiani kwa kosa dogo la kuficha taarifa za tukio hilo na kuwahukumu kifungo cha miaka minne jela.

Wawili hao walishamaliza kutumikia vifungo vyao gerezani na kurejea uraiani; mlinzi huyo akimtumia Wakili David Shillatu alikata rufaa kupinga kutiwa hatiani na adhabu ya kifo aliyopewa akiegemea katika sababu kuu mbili za rufaa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live